Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Amefungua Skuli ya Msingi ya Chanjaani Jombwe Wilaya ya Mkoani Pemba

Muonekano wa Jengi Jipya la Skuli ya Msingi Chanjani Jombwe Wilaya ya Mkoani Pemba, liliyofunguliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, ikiwa ni shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akikata utepe kuashiria ufunguzi wa Skuli ya Msingi ya Chanjaani Jombwe  Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba ikiwa ni muendelezo wa shamra shamra za kutimia miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar
Makamu wa Pili wa Rais wa zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akiondoa pazia kuweka jiwe la msingi la ufunguzi wa Skuli ya Msingi ya Chanjaani Jombwe  Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba ikiwa ni muendelezo wa shamra shamra za kutimia miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea na ujenzi wa miundombinu mbali mbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa skuli za kisasa za Ghorofa za Msingi na Sekondary  kila patakapokuwa na uhitaji ili kuimarisha kiwango cha Ufaulu kwa wanafunzi.

Ameyasema hayo wakati wa  ufunguzi wa Skuli ya Msingi ya Chanjaani Jombwe  Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba ikiwa ni muendelezo wa shamra shamra za kutimia miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Amesema kazi kubwa imeshafanywa na Serilikal ya Awamu ya Nane (8) ya kuimarisha miundombinu ya elimu katika kila Wilaya Unguja na Pemba hivyo amewataka wananchi wa Jimbo la Kiwani kuwasimamia na kuwahimiza vijana katika suala zima la kuwapatia elimu  ili kuweza kutoa wataalamu wengi na weledi watakaolisaidia na kuliongoza Taifa.

Amewataka wananchi wa Chanjaani Jombwe na maeneo jirani kuthamini maendeleo yanayoletwa na Serikali na Chama Mapinduzi kwa kuiitunza miundombinu inayoendelea kujingwa ndani ya Jimbo lao ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kuwanufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.

Mhe.Hemed ameuwagiza uongozi wa Wizara ya Elimu kuajiri walimu wazawa na  wanaoishi karibu na maeneo yanayojengwa skuli hizo ambao watasaidia kutatua changamoto ya uchelewaji na utoro wa walimu maskulini na kufanikisha azma ya Serikali ya kuondosha Zero kwa skuli za Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais amesema Serikali ipo katika mchakato wa kuzijenga barabara Kuu na Barabara za ndani kwa kiwango cha lami katika Wilaya ya Mkoani jambo litakalorahisha upatikanaji wa huduma ya usafiri, kukuwa kwa uchumi na kuongezeka kwa thamani kwa maeneo yote yatakayopitiwq na Barabara hizo.

Sambamba na hayo Mhe.Hemed  amewataka wananchi wa Mwambe na maeneo jirani kuhakikisha wanashirikiana kwa kila hali ili kuhakikisha wanapiga hatua kimaendeleo pamoja na kuimarisha amani na utulivu uliopo kwa maslahi mapana kwa vizazi vya sasa na baadae.

Nae Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Lela Mohamed Mussa amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya elimu imeweka Mifumo mbali mbali ya Elimu katika skuli za Zanzibar inakwenda kuondosha kabisa kiwango cha zero katika mitihani ya kidato cha nne(4) na kidato cha sita(6) na kuongeza  kiwango cha ufaulu nchini.

Waziri Lela amesema vifaa vyote pamoja na walimu watakaofundisha skulini hapo wapo tayari na Wizara kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) imejipanga kuitatua changamoto ya maji safi na salama kijijini hapo ili wananfunzi, walimu na wananchi waweze kunufaika na huduma hio muhimu kwa maisha ya kila siku ya binaadamu.

Akisoma Taarifa ya Kitaalamu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Ndugu Khamis Abdalla Said amesema Skuli ya Msingi Chanjaani Jombwe iliyojengwa ya ghorofa mbili(G+2) na Mkandarasi Mwinyi Building Construction imejumuisha madarasa 29, maabara, maktaba , ofisi za walimu, chumba cha Kompyuta na kumbi za mikutano hadi kumalizika kwake  imegharimu zaidi ya shilingi za Kitanzania Bilioni 4.2.

Katibu Khamis amesema kukamilika kwa ujenzi wa skuli ya Chanjaani Jombwe unakwenda kutatua changamoto ya wanafunzi kufuata skuli maeneo ya mbali panoja ambapo zaidi ya wanafunzi 1300 watapata fursa ya kujisomea katika skuli hio kwa shift ya mkondo mmoja wa asubuhi kwa wastani wa wanafunzi 45 kwa kila darasa.

Amefahamisha kuwa Madarasa yote katika skuli hio yamewekwa samani za kutosha pamoja na vifaa vya kisasa vya kusomea na kufundishia vinavyoendana na Teknoloji ya kisasa jambo litakalosaidia kunyanyua kiwangocha ufaulu ndani ya Mkoa huo.


Imetolewa na  Kitengo cha Habari ( OMPR )

Leo tarehe  02 / 01 /  2025..

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.