Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akikabidhiwa
zawadi kutoka Chuo Cha Maji mara baada ya kufungua Kongamano la Nne la Kimataifa la Kisayansi la Maji linalofanyika katika
Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam. Tarehe 29 Januari 2025. ( Kushoto
ni Waziri wa Maji Jumaa Aweso na kulia ni Mkuu wa Chuo cha Maji Dkt. Adam
Karia)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip
Mpango akishuhudia mtambo maalum wa kuchuja maji uliobuniwa na Chuo Cha Maji
wakati akitembelea mabanda mbalimbali katika Kongamano la Nne la
Kimataifa la Kisayansi la Maji linalofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City
Jijini Dar es Salaam.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip
Mpango akihutubia wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Nne la
Kimataifa la Kisayansi la Maji linalofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City
Jijini Dar es Salaam.
Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema tafiti
zinahitajika zaidi katika menejimenti ya rasilimali maji ili kuwezesha
maarifa mapya na uelewa mpana kuhusu upatikanaji na ubora wa maji
Makamu wa
Rais amesema hayo wakati akifungua Kongamano
la Nne la Kimataifa la Kisayansi la Maji lililofanyika katika Ukumbi wa Mlimani
City Jijini Dar es Salaam. Amesema ni muhimu tafiti kuelekezwa kujibu
changamoto zinazokabili menejimenti ya rasilimali za maji hususani kubaini,
kuotesha na kutunza miti ya asili ambayo inafahamika katika maeneo mbalimbali
ya kila wilaya au mikoa nchini kuwa ni rafiki wa maji.
Pia amesisitiza umuhimu wa tafiti
hizo kuangazia teknolojia rahisi, endelevu na ya gharama nafuu ya kuvuna maji
kwa ajili ya matumizi ya majumbani, sambamba na uchimbaji wa mabwawa, na kuvuna
na kuhifadhi maji ya mvua yanayotiririka kwa ajili ya umwagiliaji wa mashamba
na kukidhi mahitaji ya mifugo. Halikadhalika amehimiza umuhimu wa kuangazia
tafiti zitakazokuza kilimo janja namna bora ya kurejesha uasili wa maeneo yaliyoharibiwa na mmomonyoko
wa udongo na ukame wa muda mrefu, kubuni mifumo, mbinu na hata motisha ya
kutunza vyanzo vya maji na ardhi oevu pamoja na kuwianisha matumizi ya maji kwa
binadamu, mifugo na wanyamapori.
Aidha Makamu wa Rais ametoa rai kwa
Kongamano hilo kuangazia suala la kubuni mikakati ya kuhakikisha upatikanaji wa
maji safi na salama na huduma za uondoshaji majitaka kwa wote na kutoa
kipaumbele kwa jamii zilizo katika mazingira hatarishi. Amesema suala hilo
linapaswa kuhakikisha masuala ya mabadiliko ya tabianchi yanajumuishwa katika
mipango ya kila nchi ili kuendeleza matumizi bora ya maji na mifumo ya uondoaji
wa majitaka pamoja na kujenga uwezo wa jamii kutambua, kuhimili na kukabiliana
na matukio ya hali mbaya ya hewa.
Hali kadhalika, Makamu wa Rais
amesema majibu ya changamoto zinazohusu maji na uondoshaji wa majitaka ni
jukumu linalohitaji nguvu ya pamoja ya wadau wote wa maji ndani na jumuiya ya
kimataifa. Ameongeza kwamba kongamano hilo linapaswa kujadili namna ya kuhakikisha usalama na uendelevu wa
rasilimali za maji, utupaji sahihi wa taka za sumu na hatarishi, kuweka mifumo
endelevu ya kutenganisha aina mbalimbali za taka ngumu, matumizi ya maarifa
asilia katika menejimenti ya rasilimali
maji kama vile upandaji wa miti asilia rafiki wa maji katika maeneo ya vyanzo
vya maji na ardhi oevu.
Makamu wa
Rais amesema Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea
kuweka mazingira wezeshi yatakayo rahisisha ushirikiano katika uendelezaji wa
rasilimali maji. Aidha amewaalika watafiti na wawekezaji kutoka ndani na nje ya
nchi kushirikiana na Serikali katika menejimenti ya rasilimali maji.
Kwa
upande wake Waziri wa Maji Jumaa Aweso amesema Chuo Cha Maji kimeendelea kuwa
sehemu muhimu ya maendeleo ya sekta ya maji nchini kupitia ufundishaji na
uendelezaji wa wataalamu wa maji nchini pamoja na kutoa ushauri wa kitaalamu
ikiwemo kufanya tafiti mbalimbali ili kuondoa changamoto zinazoikabili sekta
hiyo. Amesema kongamano hilo ni sehemu ya kuimarisha upatikanaji wa mambo
mapya ikiwemo ubunifu na mbinu za
kushughulikia changamoto za maji na usafi wa mazingira nchini.
Awali
Mkuu wa Chuo cha Maji Dkt. Adam Karia amesema
kumalizika kwa kongamano hilo kutawezesha kupatikana kwa ripoti maalum
itakayotumika katika matumizi mbalimbali ya sekta ya maji na mazingira. Amesema
kutokana na umuhimu wa kongamano hilo, Chuo kimedhamiria kufanyika kwa
kongamano hilo kila mwaka ili kujadili mambo muhimu na kupelekea uelewa wa
pamoja katika masuala yote yanayohusua maji na usafi wa mazingira
Kongamano
hilo la siku tatu (29 - 31 Januari 2025) limeandaliwa na Chuo cha Maji, linawakutanisha
wadau mbalimbali wa sekta ya maji wa ndani na nje ya nchi ambalo lina kauli
mbiu isemayo “Majibu
ya changamoto za maji na uondoaji wa majitaka katikati ya mabadiliko ya
tabianchi”.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
29 Januari 2025
Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment