Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na viongozi mbali mbali, watafiti na wataalamu wa Sekta ya elimu Tanzania bara na Zanzibar kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt Hussein Ali Mwinyi katika hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Utafiti Tanzania 2025 uliofanyika katika Ukumbi wa Taasisi ya Utalii Maruhubi, Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimejipanga kuwaongezea ujuzi walimu kupitia Tehama ili kuendana na maendeleo ya Karne ya 21.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameyasema hayo kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Hussein Ali Mwinyi katika Ufunguzi wa Mkutano wa utafiti Tanzania 2025 uliofanyika katika ukumbi wa Taasisi ya utalii Maruhubi , Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).
Amesema Serikali zote mbili zimejipanga katika kuimarisha maendeleo endelevu ya walimu pamoja na kuwapatia Mafunzo yanayojukita zaidi Katika Tehama ili kuhakikisha walimu wanapata ujuzi utakaosaidia kurahisisha shughuli zao za ufundishaji.
Amesema ili kusaidia kuboresha sekta ya elimu nchini, Taasisi na wataalamu katika Sekta za elimu wana wajibu wa kuongeza nguvu katika kufanya tafiti zenye tija kwa kuangalia athari za uhaba wa walimu wa Sayansi na Teknolojia, uhandisi na hesabati (STEM) kwa matokeo ya wanafunzi na mbinu bora zitakazoweza kuziba pengo hilo.
Mhe. Hemed amesema tafiti zinazofanywa ni lazima ziangalie namna bora ya kuimarisha maendeleo ya walimu ili kuhakikisha mbinu za ufundishaji zinaendana na mahitaji ya sasa pamoja na kuhakikisha ufanisi wa mitaala inayojumuisha elimu ya tabianchi na namna ya kuboresha utekelezaji wake.
Makamu wa Pili wa Rais amesema Mabadiliko ya tabianchi ni ajenda ya dunia inayohitaji hatua za haraka kutokana na athari zake katika mazingira ikiwemo kuwa na skuli zenye miundombinu imara na mitaala inayoendana na mahitaji ya mazingira itakayowajengea wanafunzi uwelewa wa haraka.
Aidha, Mhe. Hemed amesema kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya elimu, sekta ya viwanda na Taasisi za Mafunzo ya Ufundi ni jambo muhimu ambalo litaongeza fursa za ajira kwa vijana hivyo, Taasisi husika zinapaswa kuhakikisha mfumo wa elimu uliopo unawajengea vijana ujuzi wa kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Sambamba na hayo amesema zipo changamoto zinazohitaji utafiti wa kina ili kuboresha Sekta ya elimu ya ufundi na Mafunzo ya ufundi Stadi (TVET) katika kuandaa wahitimu wa soko la ajira na mahitaji ya viwanda.
Amesema ipo haja ya kuangalia namna bora ya kuimarisha mitaala ya TVET ili kuhakikisha inakidhi mahitaji ya soko la ajira linalobadilika kwa kasi pamoja na kufanya utafiti wa matumizi ya TEHAMA na Teknolojia bunifu katika kuboresha mafunzo ya ufundi na ufanisi wa utoaji wa elimu ya TVET.
Nae Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Lela Mohamed Mussa amesema Kongamano hilo litajadili elimu ya mafunzo ya amali ambayo kwa upande wa Zanzibar imekuwa ni sehemu ya elimu ya kawaida ili kuwajengea uwezo vijana wanapomaliza masomo yao kuweza kubuni kazi za kufanya na kujiajiri badala ya kusubiria kuajiriwa na Serikali ama Taasisi nyenginezo.
Mhe. Lela amesema Serikali zote mbili ni sikivu hasa katika suala la maendeleo hivyo, zitakuwa tayari kupokea matokeo ya Kongamano hilo kwa ajili ya kuboresha na kuimarisha sekta ya elimu Nchini Tanzania.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) Profesa Mohamed Makame Haji amesema lengo la Kongamano hilo ni kuangalia namna bora ya kuimarisha Elimu ya juu kwa kutafuta mbinu mbali mbali za kuwanyanyua Walimu kitaaluma kwa kuwaongezea ujuzi na mbinu shirikishi za kufundishia kwa maslahi mapana ya sekta ya elimu Nchini.
Profesa Makame amesema Kongamano hilo litatoa fursa kwa watafiti, wasomi na wadau wa elimu kukaa pamoja na kujadili mafanikio na changamoto zinazoikabili Sekta ya elimu ya juu Tanzania na kutafuta suluhisho la changamoto hizo.
Amesema SUZA kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Taifa cha Dar es Salaam (UDSM) na wadau mbali mbali wa sekta ya elimu wamejipanga kuimarisha ufanyaji wa Tafiti, matumizi ya Tehama na Programu mbali mbali ili kuona matokeo ya Tafiti hizo yanatumika ipasavyo katika sekta mbali mbali nchini.
Kamishna wa elimu Tanzania Profesa Lyambwene Mtahabwa amesema Sera ya Elimu Tanzania inatambua kiini cha mafanikio katika sekta ya elimu ni Mwalimu bora hivyo, suala la maslahi ya Walimu na kuwajengea uwezo kitaaluma na kiubunifu limeangaliwa kwa kina kwa mustakbali wa Sekta ya elimu Tanzania.
Profesa Mtahabwa amesema wakati umefika kwa Taasisi za Elimu nchini kutambua ujumuishaji wa Wanafunzi wenye mahitaji maalum pamoja na kutoa hamasa kwa walimu ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa.
Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)
Tarehe 25.02.2025
......................................................................
No comments:
Post a Comment