WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali inatambua na kuthamini kazi inayofanywa na viongozi wa dini pamoja na wa kimila katika kuhakikisha nchi inakuwa na ustawi wa jamii.
Amesema ni jambo la faraja kuona wakati wote viongozi hao wamekuwa wakifanya kazi na kuvuka mipaka ya kiroho na kugusa ustawi na maendeleo ya jamii katika nyanja mbalimbali.
Ameyasema hayo leo Jumatano (Februari 26, 2025) alipomwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Maadhimisho ya Siku ya Maridhiano ( Maridhiano Day), iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) Mkoani Arusha.
"Serikali inatambua na kuthamini mchango wenu mkubwa katika kufanikisha masuala muhimu ya kitaifa yanayowaunganisha Watanzania wote, ikiwemo uhamasishaji wa waumini katika kampeni mbalimbali muhimu kwa Taifa. Ninawasihi endeleeni kutoa ushirikiano huo kwani sauti zenu zina nguvu kubwa katika jamii."
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa viongozi hao kuendelea kushirikiana na Serikali katika kudumisha amani ili Watanzania waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali.
"Ninatambua JMAT iko kwa lengo hilo, hivyo endeleeni kuongeza wigo wa kuhamasisha na kudumisha upendo, amani umoja na mshikamano hapa nchini."
Amesema suala la kudhibiti mmomonyoko wa maadili limeendelea kuwa ajenda ya kudumu ya viongozi hao. "Ninawasihi sana endeleeni kukemea vikali vitendo vyote ambayo ni kinyume na maadili ya dini na utamaduni wa Mtanzania."
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amesema Falsafa ya 4R iliyoasisiwa na Rais Dkt. Samia imekuwa chachu katika kuimarisha Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Mabadiliko hivyo kujenga jamii ya Watanzania yenye Amani, Umoja, Mshikamano.
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amemuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Manyara kupitia Ikama na kupeleka watumishi katika kituo cha afya kilichojengwa na Jumuiya hiyo katika eneo la Simanjiro.
Kwa Upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania, Dkt Alhad Mussa Salum amesema Jumuiya hiyo itaendelea kuiunga mkono Serikali katika shughuli mbalimbali huku akitoa wito kwa viongozi wa dini kuendelea kuifanya kazi yao kwa hofu ya Mungu ili kuendelea kujenga amani na ustahimilivu.
Naye, Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda amesema Jumuiya hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika kujenga amani, upendo na ustahimilivu miongoni mwa Watanzania na kuomba Serikali iendelee kuiunga mkono Jumuiya hiyo.
"Viongozi hawa wanafanya kazi kubwa ya kujitolea katika kujenga amani ya nchi yetu, ni muhimu sasa Serikali kuendelea kuiunga mkono jumuiya ili jitihada zao ziendelee kuonekana."
Kwa Upande wake, Mjumbe, wa Kamati ya JMAT Taifa na Spika Mstaafu, Anna Makinda ametoa wito kwa viongozi wa vyama vya siasa kuhubiri amani na kuacha kufanya siasa ambazo zinaweza kuwagawa Watanzania na kuhatarisha amani, upendo na mshikamano.
Maadhimsho hayo yameandaliwa na Jumuiya Ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT).
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, FEBRUARI 26, 2025.
No comments:
Post a Comment