Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla Amekabidhi Iftaar kwa Wanafunzi Wanaokaa Katika Dahalia Zanzibar

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akikabidhi Iftari kwa walimu na wanafunzi Wanaoishi Dahalia kwa skuli ya Sekondari Lumumba iliyopo Wilaya ya Mjini Unguja.


Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka kipaombele katika Sekta ya Elimu  kwa kuandaa mazingira wezeshi ya kuhakikisha Wanafunzi wote wanaopata fursa ya kujiunga na Elimu ya juu wanapatiwa Mikopo ili kuweza kuendelea na masomo yao pasipo na changamoto ya ada.

Hayo yamesemwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla wakati wa ziara yake ya kuwatembelea na kuwapatia sadaka ya Iftari Wanafunzi wote wanaoishi dakhalia katika skuli zote za Unguja na Pemba ikiwa ni kawaida yake kila ifikapo mwezi mtukufu wa ramadhani kufanya hivyo kwa kila mwaka.

Amesema Serikali  imetenga Bajeti ya zaidi ya Bilioni 33 kwa ajili ya kuwasomeshea Wanafunzi watakaojiunga na elimu ya juu kuanzia ngazi ya Diploma hadi shahada ya uzamivu hivyo, amewataka Wanafunzi kuongeza  bidii katika masomo yao ili kuweza kunufaika na fursa hiyo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema lengo la kuwapatia Wanafunzi Iftari hio ni kuwasaidia ili kuweza  kuendeleza funga zao pasipo na changamoto ya Iftari na kupata fursa ya  kusoma katika hali ya utulivu wa kila jambo.

Aidha Mhe.Hemed  amewapongeza Walimu kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuwasomesha na kuwasimamia Wanafunzi kimalezi na kimaadili  na kuwaahidi kuwa Serikali itaendelea kuwaangalia Walimu kimaslahi kadiri hali itakavyoruhusu.

Nae Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Lela Mohamed Mussa amemshukuru Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa wema na  upendo wake alionao kwa wanafunzi kwa kuwapatia Iftari wanafunzi wanaokaa dakhalia  kila ifikapo mwezi mtukufu wa ramadhani jambo ambalo litaendelea kuacha alama ndani ya mioyo ya wanafunzi hao na Wazanzibari kwa ujumla.

Waziri Lela amesema Serikali imeweka mazingira mazuri na rafiki kwa Wanafunzi ya kuweza kujisomea jambo ambalo linaongeza ari na hamasa kwa Wanafunzi kuweza kufanya vizuri katika mitihani yao ya Taifa na kuongeza kiwango cha ufaulu nchini.

Amempongeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa kutenga muda wa kuonana na Wanafunzi na kuzungumza nao  pamoja na kuwatia moyo wa kusoma kwa bidii ili waweze kufanya vizuri katika masomo yao.

Akizungumza kwa niaba ya Wakuu wa Mikoa mitatu ya Unguja, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mhe. Mattar Zahor Massoud amesema viongozi wa Mikoa wamejipanga kuhakikisha wanakuza viwango vya ufaulu na kuhakikisha wanafuta daraja la zero ndani ya Mikoa yote ya zanzoibar ili kuendana na matakwa ya Serikali ya Awamu ya Nane (8) ya kuondoa divisheni zero kwa skuli zote za Zanzibar.

Zahor amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri katika Sekta ya Elimu ili kuhakikisha Wanafunzi wanasoma katika mazingira bora hivyo, juhudi za pamoja zinahitajika katika kuunga mkono jitihada hizo za Serikali ili kuweza kukuza kiwango cha ufaulu ndani ya Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Akitoa shukurani kwa niaba ya Wanafunzi wenzake, Mwanafunzi wa kidato cha Sita ( 6) kutoka Skuli ya Sekondari Mkokotoni   Asya Mussa Ali ameishukuru Serikali ya Awamu wa Nane (8) kwa kuimarisha miundombinu ya Elimu na kuwajengea Skuli ya gorofa iliyosheheni  vifaa vyote vya kusomea na kufundishia.

Aidha amemshukuru Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa kuona umuhimu wa kuwatembelea na kuwafutarisha kila ifikapo Mwezi wa Ramadhani jambo ambalo linawapa hamasa ya kusoma kwa bidii na kuweza kufanya vizuri katika masomo yao.

Skuli zilizotembelewa na Makamu wa Pili wa Rais na kupatiwa sadaka ya Iftari ni pamoja na Chuo cha Kiislam Mazizini,Skuli ya Sekondari Donge, Mkokotoni,Mkwajuni, Mtule na Hasnuu Makame.

 

Imetolewa na kitengo cha Habari ( OMPR )

Leo tarehe 18 / 03 / 2025.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.