MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amesema serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na chama cha madaktari bingwa wa magonjwa ya kizazi na uzazi Tanzania (AGOTA).
Mhe. Hemed ameeleza hayo kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwenye ufunguzi kongamano la kisayansi lililoandaliwa na AGOTA, chama cha kitaaluma cha ISGE kwa kushirikiana na wizara ya Afya.
Alisema madaktari bingwa wa magonjwa ya kizazi na uzazi, wamekuwa nguzo muhimu katika kusaidia mipango mbalimbali ikiwemo juhudi za kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga nchini Tanzania.
Alisema mabadiliko ya tabianchi yamekuwa kichocheo cha kuibuka kwa maradhi ya mripuko na kuongezeka kwa magonjwa yasiyoambukiza, hivyo kuna umuhimu wa kuzalisha wataalamu wa afya watakao ongoza katika kukabiliana na hali hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amevipongeza vyama vya kitaaluma kama AGOTA na ISGE kwa kushirikiana na vimekuwa na mchango kwenye mambo mbalimbali ikiwemo kwenye utungaji wa sera na miongozo yenye lengo la kuimarisha utoaji wa huduma bora za kiafya kwa mama wajawazito na watoto.
Aidha, alifahamisha kuwa kongamano hilo limelenga katika kuboresha na kuimarisha huduma za uzazi na tiba za magonjwa ya kizazi na kusaidia katika kuimarisha huduma za afya, elimu na tafiti
nchini.
Sambamba na hilo, aliwataka wataalamu wa afya kuendelea kufanyakazi kwa juhudi, maarifa na uweledi ili kuendelea kuleta mageuzi katika sekta hiyo, ambapo aliwahakikishia kuwa serikali itaendelea kutoa ushirikiano katika kutatua changamoto zinazoikabili sekta hiyo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Hassan Khamis Hafidh, alisema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, inaendelea kuipa kipaombele sekta ya afya hasa kwenye utoaji wa huduma za mama waja wazito na watoto kwa lengo la kupunguza vi fo vya uzazi.
Naibu Waziri aliishukuru AGOTA kwa kushirikiana na wizara ya Afya kwa kuandaa kongamano hilo la kisayansi ambalo linawakutanisha wataalamu wa afya hasa kada ya uzazi na kizazi ambao watajadili mafanikio, changamoto na namna ya kukabiliana nazo.
Akimwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Afya Tanzania, Dk. Mzee Nassor aliesema ili Tanzania iweze kufikia mafanikio katika sekta ya Afya ni lazima kuwepo na mashirikiano makubwa kati ya serikali, wataalamu na wadau katika kusimamia na kuimarisha masuala ya tiba, vifaa tiba na kujifunza teknolojia mpya inayoendana na mabadiliko ya huduma za afya kidunia.
Dk. Nassor alisema Wizara ya Afya inathamini jitihada zinazochukuliwa na AGOTA katika kuhakisha upatikanaji wa huduma bora za afya nchini kwa kushirikiana na Serikali katika kutatua changamoto mbali mbali na kubuni njia bora za kupambana na changamoto hizo ikowemo kuandaa sera, tafiti na mikakati madhubuti ya kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za Afya nchini.
Naye rais wa chama cha madaktari bingwa wa magonjwa ya kizazi na uzazi Tanzania, Dk. Matilda Ngarina, alisema AGOTA itaendelea kushirikiana na serikali na wadau wa sekta ya afya kwa kufanya tafiti, kuandaa sera na kubuni miradi inayolenga kuimarisha huduma za afya na upatikanaji wa matibabu kwa wananchi.
No comments:
Post a Comment