Habari za Punde

Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF) Yapongezwa kwa kazi kubwa inazoendelea


MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, ameipongeza Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), kwa kazi kubwa inazoendelea kuzitekeleza zikiwemo afya, elimu na uwekezaji ambazo zinalenga kukuza ustawi wa jamii.

Ameyameeleza hayo wakati alipofanya mazungumzo na uongozi wa taasisi hiyo uliofika ofisini kwake Vuga, kwa ajili ya kumpongeza kwa majukumu anayoyatekeleza ya kumsaidia Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Mhe. Hemed amesema malengo ya ZMBF yanajieleza wazi nayo ni kusaidia ustawi wa jamii, hivyo ameipogeza taasisi hiyo kutokana na utatuzi wa changamoto zinazogusa maisha ya wananchi.

Ametumia fursa hiyo kumpongeza Mwenyekiti wa ZMBF, Mama Mariam Mwinyi kwa kazi kubwa inayofanywa na taasisi yake ambayo inafanya kazi na makundi mbali mbali ikiwemo wanafunzi, wanawake na watoto, jambo linaloakisi dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Amefahamisha kuwa Taasisi hiyo imekuwa ikiwafikia wananchi moja kwa moja katika maeneo yao na kuwapatia huduma ya matibabu bure sambamba na kufuatilia maendeleo yao baada ya kupatiwa matibabu hayo.

Makamu wa Pili wa Rais, amesema yuko tayari kutoa kila aina ya mashirikiano ili kuhakikisha uzinduzi wa kambi ya tano ya afya bora maisha bora inafanikiwa kwa kiwango kikubwa na kuwafikia walengwa.

Kwa upande wake, ofisa mtendaji mkuu wa ZMBF, Fatma Fungo amesema taasisi hiyo inaendelea na kampeni yake ya afya bora maisha bora yenye lengo la kutambua changamoto za kiafya zinazowakabili wananchi wa Zanzibar.

Mtendaji huyo alisema kampeni hiyo imeshafanyika kwenye mikoa minne ya Zanzibar na wanatarajia kukamilisha katika Mkoa uliobakia wa Kusini Pemba kuanzia Agosti 11 hadi Agasti 15 mwaka huu.

Fungo alisema kambi hizo za matibabu bure zimekuwa zikitoa matokea chanya na wananchi wamekuwa wakijitokeza kwa wingi katika kufanya uchunguzi wa afya zao na kupatiwa matibabu mbali mbali.

Naye ofisa mratibu wa huduma za Afya wa ZMBF, Ibrahim Issa ameesema uzinduzi wa kambi ya afya bora maisha bora, inatarajiwa kufanyika katika viwanja vya hospitali ya Vitongoji Pemba ambapo wananchi watapata fursa ya kuchunguza afya zao kwa kufanya vipimo vya awali, sambamba na kupatiwa ushauri.

Issa alizitaja huduma nyengine zitakazotolewa katika kambi hio kuwa ni pamoja na upasuaji mdogo, huduma ya mama na mtoto, matibabu ya magonjwa ya kansa na uchangiaji wa damu wa hiari ili kuendelea kuokoa vifo vya wazanzibari wengi vinavyochangiwa na kupoteza damu.

Kambi ya tano ya Afya bora maisha bora iliyoandaliwa na Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation, inatarajiwa kuzinduliwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, ambapo madaktari bingwa wakisaidiana na wataalamu mbali mbali wa afya watatoa huduma.

Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)
Tarehe 30.07.2025



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.