Ameyasema hayo kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, katika maadhimisho ya siku ya vijana kimataifa yaliyofanyika skuli ya sekondari Utaani Wete, Pemba.
Amesema malengo ya maadhimisho hayo ni kutambua na kuthamini mchango wa vijana katika maendeleo ya taifa na kufanya tathmini ya mafanikio na changamoto zao, ili zipatiwe ufumbuzi.
Mhe. Hemed amesema serikali imeimarisha usimamizi na uratibu wa shughuli za maendeleo ya vijana kwa kusambaza na kujenga uelewa wa sera ya maendelo ya vijana ya mwaka 2023 kwa wadau wa maendeleo.
Aidha amefahamisha kuwa kwa sasa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, inaandaa sera hiyo kwa lugha nyepesi ili kuwasaidia vijana kuielewa.
Aidha, Mhe. Hemed amesema Wizara imetenga shilingi bilioni 16.5 kwa ajili ya miradi ya vijana ikiwemo kuwekeza katika vituo vya maendeleo na kusaidia miradi ya kiuchumi yakiwemo mabaraza ya vijana.
Katika kuwawezesha vijana kiuchumi, amesema serikali inaendelea kuimarisha fungu la vijana la mkopo kupitia ‘4.4.2’ ambapo kwa sasa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi umeweka mfumo wa maombi kupitia mtandao.
Sambamba na hayo ameeleza katika kukuza ajira kwa vijana, serikali imeanzisha mradi wa SEBEP ili kuwapatia ujuzi wa kujiajiri na kuajiriwa katika sekta ya uchumi wa buluu kupitia vituo vya amali.
Ili kufanikisha hilo, amesema serikali itajenga vituo vyengine saba vya amali na kuandaa mtaala maalum wa ajira kupitia uchumi wa buluu utakaotumika kufundishia.
Pia serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ya michezo kwa kufanya matengenezo ya viwanja vya zamani na kujenga vipya katika ngazi ya wilaya, mkoa na taifa ili kukuza sekta hiyo.
Nae Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita, amesema siku ya vijana kimataifa inatoa fursa kwa vijana kujitathmini, kushugulikia changamoto zilizojitokeza na kuangalia mbele kwa mafanikio zaidi ili kutimiza malengo yao.
Amemshukuru Rais Dk. Hussein Mwinyi kwa kuwapa kipaombele vijana na kuwapatia fursa ikiwemo kuwateuwa kushika nyadhifa mbalimbali serikalini.
Amesema vijana wapo tayari kufanya maamuzi ya kuchagua na kuchaguliwa na kuhakikisha wanafanya maamuzi sahihi ya kumpigia kura za kishindo na kumeejesha madarakani ifikapo mwezi Oktoba.
Mjumbe wa Baraza la Watendaji Taifa kutoka Baraza la Vijana, Asila Yussuf Hamad, amesema vijana wanashuhudia juhudi zinazofanywa na serikali katika kuimarisha maendeleo na ustawi wa vijana.
Amesema juhudi hizo zimeleta matokeo chanya ikiwemo ongezeko la wasomi na mikopo nafuu ya kuwawezesha vijana kujiendeleza.
Amefahamisha kuwa katika serikali ya awamu ya nane vijana wanashirikishwa katika ngazi za maamuzi na kuaminiwa kushika nyadhifa za uongozi.
Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)
Tarehe 12.08.2025
No comments:
Post a Comment