SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, inakusudia kujenga vituo vya kisasa kila wilaya vitakavyotumika kusambaza mbinu za kisasa za kilimo, mifugo na misitu kuanzia uzalishaji hadi usarifu wa mazao.
Hayo yamesemwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, katika hafla ya ufungaji wa maonesho ya kilimo ya nane nane, katika viwanja vya Kizimbani wilaya ya magharibi ‘A’ Unguja.
Amesema kampuni ya Uingereza itajenga vituo hivyo ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa mageuzi ya kilimo Zanzibar wa mwaka 2025/2030.
Aidha, amefahamisha kuwa utekelezaji mpango huo ni jambo la msingi na la kupewa kipaumbele ili kuimarisha kilimo kutoka kikimo cha kujikimu hadi kilimo cha biashara kwa lengo la kuleta tija kwa wananchi.
Mhe. Hemed amesema serikali inachukua juhudi kuhakikisha kilimo kinaendelea kuimarika kwa kuimarisha miundombinu ya mwagiliaji katika mabonde saba Unguja na Pemba ambayo imeongeza tija katika uzalishaji wa mpunga kutoka wastani wa tani tatu kwa hekta hadi tani 11.
Ameelezea dhamira ya serikali ya kuleta mageuzi ya kilimo kwa kuwa sekta hiyo ni kiungishi cha sekta nyingi muhimu kama biashara, viwanda, utalii, afya, ajira, uwekezaji, mazingira, maji na nishati.
Sambamba na hayo serikali inaendelea kuwapatia wakulima pembejeo za kilimo ikiwemo mbegu, mbolea, dawa, matrekta na huduma nyengine kama elimu kwa wakulima na kufanya tafiti.
Amepongeza hatua ya kuanzishwa televisheni ya kilimo inayowasaidia kuwaunganisha wakulima, wataalamu na wadau wa wengine wa kilimo kwa lengo la kutoa elimu, taarifa na kusambaza mbinu za kisasa ili kuendana na hali ya soko.
Ameiagiza Wizara ya kilimo, Maliasili na Mifugo, kuendelea kuwa karibu na wadau wakilimo, wakulima na wafugaji kwa kusimamia ipasavyo sera, programu na mikakati ya kilimo ili kuleta ufanisi zaidi.
Kwa upande wake, Waziri wa wizara hiyo, Shamata Shaame Khamis, amesema wizara itahakikisha wananchi hasa wakulima na wafugaji wanapata huduma kwa wakati na kwa unafuu.
Ameipongeza serikali ya awamu ya nane kwa kuipa kipaombele sekta ya kilimo kwa kujenga masoko ya kisasa yaliyokidhi viwango kwa wafanyabiashara ambayo yanatoa fursa kwa wakulima na wafugaji kupata sehemu salama ya kuuzia na kufanyia biashara zao.
Amefahamisha kuwa miundombinu ya barabara inayojengwa nchini ni chachu ya wakulima na wafugaji kupata urahisi wa kufikisha bidhaa zao mashambani na masokoni zikiwa katika hali ya ubora.
Shamata amesisitiza kuwa wizara itaendelea kuwahamasisha wakulima na wafugaji kulima na kufuga kisasa na kutumia pembejeo rafiki ambazo huwawezesha mkulima kulima kilimo chenya tija zaidi.
Akiwasilisha taarifa ya maonesho hayo, Katibu Mkutano Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Ali Khamis, amesema maonesho hayo yamezidi kuwa na mwitikio ambapo washiriki 400 wameshiriki kutoka Zanzibar na Tanzania Bara jambo linalotoa hamasa kwa wizara kuendelea kuyaimarisha.
Amesema wizara imefanikiwa kuanzisha televisheni inayojuulikana kwa jina la Kilimo TV inayofuatiliwa na wananchi wengi kuangalia vipindi na kupata elimu ya kilimo na ufugaji wa kisasa.
Ameishukuru serikali kwa kuwezesha kufanikisha maonesho hayo ambapo julma ya shilingi za bilioni moja zimetolewa na kutumika kwa kuimarisha miundombinu katika eneo la maonesho.
Amewapongeza wadau na washiriki wakiwemo wakulima, wafugaji na taasisi mbali mbali kwa mwitiko wao mkubwa uliosaidia kufanikisha maonesho hayo.
Nao washiriki, wamesema kupitia maobesho hayo wanajifunza mambo mbali mbali ikiwemo mbinu bora na rafiki za kilimo na kufuga kidijitali.
Wameiomba serikali kuendelea kuyaimarisha maonesho hayo kwa kujenga miundombinu, kuongeza elimu na taaluma kwa wakulima na wafugaji na kuhakikisha upatikanaji rahisi wa pembejeo.
Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)
Tarehe 14.08.2025
No comments:
Post a Comment