Habari za Punde

MSHINDI MAISHA PLUS KUTINGA BUNGENI


Na Donisya Thomas -- ZANZIBAR LEO


MSHINDI wa shindano la Maisha Plus Abdulhalim Hafidh Salum, leo anatarajiwa kuwasili mjini Dodoma kuitikia wito wa Spika Samuel Sitta, kumtaka ahudhurie bungeni kutambulishwa.


Spika Sitta alitoa mualiko huo juzi alipokuwa akiwatambulisha washiriki wengine wa shindano hilo lililomalizika kwa Salum kutwaa ushindi na kutia kibindoni shilingi 10,000,000.



Sitta amemtaka mshindi huyo kufika katika afisi za bunge ili aweze kupokewa kwa heshima zote kutokana na ushindi huo mwanana pamoja na kujionea shughuli mbali mbali za bunge.


"Yuko wapi Abdulhalim, mbona hamjamleta tukamuona, mleteni bwana tumuone mshindi wetu wa Maisha Plus", aliuliza Spika katika utambulisho huo.


Akizungumza na gazeti hili, Salum alisema amepata mualiko rasmi kumtaka kwenda Bungeni na ameupokea kwa mikono miwili.Alisema hiyo ni heshima kubwa kwake pamoja na Zanzibar, kwamba hata Mtendaji Mkuu wa Afisi ya Bunge amemtambua na kumpatia nafasi hiyo adhimu.


"Ni kweli nimealikwa Bungeni, nimepokea simu leo (jana) mchana nikitakiwa nihudhurie huko nami niko njiani, Mungu akipenda kesho nitakuwepo Dodoma", alisema.


Abdulhalim Hafidh alikuwa miongoni mwa washiriki 53 walioshindana katika kijiji cha Maisha Plus na kutwaa donge nono la shilingi 10,000,000 baada ya kuibuka mbele ya washindani wengine.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.