Na Ally Saleh
Sijawahi kufanana nae kwa hali yoyote. Tulikuwa tumepishana kiumri kiasi mimi ni wa kizazi chengine na yeye wa chengine kabisa na hilo kwa siasa na hali ya kijamii ya Zanzibar ni muhimu sana. Sina sifa ambazo zinaweza kumfikia kwa namna yoyote ile. Mimi ni kichuguu na yeye ni mlima.
Kama walivyo watu wengi wa kizazi changu waliowahi kupitia Chuo Kikuu cha Dar es salaa, Profesa Haroub alikuwa mwalimu wetu. Na ndie yeye aliye tuendesha tata ya uchambuzi wa masuala ya siasa na jamii. Tunamkubuka wengi alivyokuwa akijiamini kwa kuingia kutoa mihadhara akiwa na kipande cha karatasi lakini mambo yakatiririka kama maji katika mlima.
Sehemu kubwa ya maisha yangu nilikuwa natamani kuwa kama yeye mpaka pale ndoto zangu zilisokotwa na maamuzi ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam kuninyima fursa ya kupata digrii yangu ya pili ya sheria hata baada ya kukamilisha kuandika kazi yangu mwaka 1996. Kwa hivyo sitakuwa professa kama alivyokuwa Profesa Haroub.
Sifichi kuwa Professa Haroub alikuwa ni kichocheo cha maisha yangu nikitegemea kufikia kiwango cha elimu kama yeye, lakini pia alikuwa ni msukumo wangu na kutamani kufikia kiwango cha kujitolea katika jamii kama yeye. La muhimu zaidi ni kutamani kuwa kama yeye katika suala la kusimamia haki.
Tulitofautiana kwa mawazo katika mambo kadhaa na sikuficha kumwambia na kitu ambacho siku zote kilikuwa kinanishangaza ni namna ambavyo alivyokuwa akipokea mawazo yasiokubaliana na yeye bila hata ya uso wake kubadilika.
Nafikiri ilijiwekea kanuni muhimu katika maisha kwamba maisha ni kukosolewa hata ufikie kiwango gani cha usomi au nafasi katika jamii. Hii ilikuwa ni sifa muhimu sana kwa Professa Haroub.
Tuliwahi kukutana katika majukwaa kadhaa ambapo tulitoa hoja ya mambo ya Muungano wa Tanzani, chaguzi za Zanzibar, mambo ya sheria na mengine mengine. Tuliwahi kusafiri pamoja na kuwa katika jukwaa moja hata nje ya nchi.
Imetokea hata mimi nae tuliwahi kulala chumba kimoja kwa zaidi ya wiki moja wakati tulikupokuwa katika ziara ya Marekani katika jimbo la Texas na California. Na hapa ndipo nilipomjua sana mtu ambaye kwa umri wetu nisingeweza kumkaribia na kujua mambo kadhaa.
Mtu yoyote yule aliyewahi kufanya kazi na Professa Haroub atamjua kwa usatahamilivu wake, uwezo wake wa uchambuzi wa masuala mbali mbali na umakini wake katika kusikiliza. Sifa yake kusikiliza ilikuwa muhimu sana katika maamuzi yake mengi.
Mimi sio katika watu waliomjua Professa Haroub zamani sana. Lakini kwa muda nilomjua kwa maana ya kufanya nae kazi pamoja najua jinsi anavyo heshimu watu kwa umri wao na hata kwa kiwango chao cha elimu na hadi kiwango chao cha uelewa. Hajawahi kupiga mstari wa kupendelea mawazo ya wasomi na akiwaacha wananchi.
Lakini rangi halisi za Professa Haroub zimejitokeza tokea alipoanza kusimamia taasisi ya Kituo cha Sheria cha Zanzibar ZLSC na kabla ya hapo pale aliposimamia taasisi ya kufuatilia uchaguzi Zanzibar kwaka 1995 katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi hapa Zanzibar yaani ZEMOG.
Hapo ndipo mitizamo na misimamo yake kadhaa ilipoimarika juu ya suala la haki hapa Zanzibar.
Huko nyuma wengi walimhusisha Professa Haroub na siasa au tuseme uhafidhina na kuthubutu hata kusema kuwa hakuwa jasiri katika kusimamia haki na kuwa alikuwa akilinda kitumbua chake kwa kuwakingia kifua wakubwa katika maovu yao kwa jamii.
Huko nyuma wengi walimhusisha Professa Haroub na siasa au tuseme uhafidhina na kuthubutu hata kusema kuwa hakuwa jasiri katika kusimamia haki na kuwa alikuwa akilinda kitumbua chake kwa kuwakingia kifua wakubwa katika maovu yao kwa jamii.
ZEMOG ilimpa nafasi ya kuonyesha kuwa anaweza kunyooshea kidole taasisi yoyote ile isiyofuata maadili na haki. Anaweza kukemea upotoshaji wa sheria na katiba na kuwa pia anaweza kuiambai Serikali na chama chochote kuwa maslahi ya nchi ni muhimu zaidi kuliko kitu chengine chochote.
Kwa miaka mitatu ZLSC imekuwa ikishirikiana na kituo cha katiba na haki za binaadamu cha Tanzania LHRC kutoa ripoti za mwaka za hali ya haki za binaadamu hapa Zanzibar. Ni ripoti hizo ambazo zitaanza kuwa thamini sasa maana ni chini ya uongozi wake mengi yamesemwa.
Kwa miaka mitatu Serikali ya Zanzibar imekuwa ikisusia uzinduaji wa ripoti hizo.
Kwa miaka mitatu Serikali ya Zanzibar imekuwa ikisusia uzinduaji wa ripoti hizo.
Ya mwisho kabisa iliotolewa miezi miwili iliyopita Professa Haroub alizungumzia sana suala la mgogoro wa ardhi ambao unainyemelea Zanzibar akionya kuwa hatua isipochukuliwa nchi itaingia katika machafuko.
Mnasaba na ardhi, miezi mitano nyuma Professa Haroub alilivalia njuga suala la kuvunjiwa nyumba wakaazi kadhaa wa eneo moja hapa Zanzibar na alikuwa mkali sana kuwa hatua ilichukuliwa ilhali kukiwa na shauri mahakamani jambo ambalo litakuwa limeeleza jinsi Serikali ya Zanzibar isivyoheshimu utawala wa sheria.
Kwa waandishi wengi wa habari Professa Haroub alikuwa ni chanzo kikubwa cha taarifa. Wakati wowote alikuwa tayari kuzungumza na waandishi wa habari kwa kujua kuwa neno lake lina sauti katika jamii na kuwa hakupaswa kulifanyia hiyana neno hilo.
Mwezi mmoja unusu nyuma nilipata nafasi ya kufanya nae kazi katika kile tulichokiita kuandaa sherehe ya kumkumbuka marehemu Khalfan Hemed Khalfan ambaye alikuwa ni mjumbe wa Bodi ya ZLSC lakini pia aliyetoa mchango mkubwa katika masuala ya haki za walemavu Zanzibar, Tanzania na Duniani.
Madhumuni yalikuwa ni kujenga tabia ya kuwaenzi watu ambao wameifanyia mema jamii ili na wengine wajue kujitolea kwao hakutakuwa bure baada ya vifo vyao, bali jamii itawakumbuka nae Professa Haroub alisema kifo cha Maalim Khalfan kisifanywe kuwa msiba bali ni sherehe kwa aliyofanikiwa kuyafanya.
Hatukujua kuwa baada ya kutoongoza katika sherehe hizo basi atakuwa ni yeye ambaye atafuatia katika kumfanyia sherehe za mafaniko yake ambaye kwa hakika ni mengi kupita kiasi kuamini kuwa yamefanywa na mwanaadamu katika umri mmoja tu.
Juzi Jumamosi alikuwa ni mchambuzi katika uzinduzi wa kitabu kilichojikita katika maisha ya wanasiasa wawili maarufu wa Zanzibar, Ali Sultan Issa aliyekuwa mwanachama wa Zanzibar Nationalist Party au Hizbu na baadae Umma Party na pia Waziri katika Serikali ya Mapinduzi mwaka 1964 na katika Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF Seif Shariff Hamad.
Alisema mengi ikiwa ni pamoja na kuhimiza suala la kusahemeana na kujenga umoja wa Wazanzibari lakini pia pembezoni akamtolea wito aliyekuwa mgeni rasmi Dk Salim Ahmed Salim aandike kitabu juu ya maisha yake. Kwa hakika ilikuwa ni kama kusikitika kuwa yeye hakuwa tena na muda wa kuandika kitabu juu ya maisha yake maana saa 24 baadae alituondokea.
Ni wazi kuwa mwanazuoni mkubwa sana wa Kizanzibari anayeijua siasa na hali nzima ya Zanzibar ametuondokea. Ni wazi mwanaharaki mkubwa aliyetetea haki za wanyonge wa Afrika Kusini, Palestina, Zimbabwe na kwengine ametuondokea. Ni wazi kuwa mwalimu aliyefunza watu wengi ametuondokea na ni wazi kuwa msemaji wa haki za wanyonge wa Zanzibar ameondoka.
Ni kweli kuwa kuna imani kuwa paondokapo panajazwa lakini si rahisi kumpata mtu aliyefikia kilele cha elimu ikisha akakubalika katika jamii kwa sauti na matendo yake, kwa wema na maelewano kama alivyofikia Professa Haroub.
Kwa baadhi yetu kufa kwake kumetuzidishia matumaini. Kwamba amekufa kukiwa bado kuna mengi ya kufanya na kutuzindua kuwa bado hatujafanya tunayopaswa kuyafanya kulinda uhuru wetu, kuhimiza demokrasia na kujenga nchi yetu.
Alichofanya Professa Haroub katika umri wake ilikuwa ni kutoonyesha njia kwa kutushika mkono. Kutuongoza ili tukue na tujue tunakoelekea na wengi tuliokuwa wanafunzi wake darasani na waliohusudu nje ya darasa sasa tumeshajua njia…na naamini tutakuwa nyuma yake.
Kwangu Professa Haroub hajafa bali ametangulia tu, maana kufa ni kuzikwa na kusahauliwa na yeye amekufa tu lakini ataishi milele na kwa hivyo kuwepo kwake katika nyoyo zetu ni sawa kuwa ametutangulia tu.
No comments:
Post a Comment