Habari za Punde

WAPONGEZWA KWA KUOKOA MALI, MAITI

Na Mwandishi Wetu


WAPIGANAJI wa vikosi vya ulinzi wamepongezwa kwa kazi kubwa ya kuokoa mali na maiti za watu waliozama katika meli ya Mv. Fatih. Pongezi hizo zilitolewa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, wakati akizungumza na wapiganaji wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania na vikosi vya SMZ, walioshiriki kazi ya kukwamua meli hiyo.


Dk. Mwinyi alisema wapiganaji hao walifanya kazi kubwa katika kipindi cha wiki moja, kuhakikisha kazi hiyo inafanikiwa bila ya kujali muda na mazingira magumu ya kazi. Waziri huyo, ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Mikunguni, alifika eneo la bandari ya Malindi kuangalia kazi zilizokuwa zikifanyika za kuopoa maiti na meli ya Fatih iliyozama wiki moja iliyopita.


Uongozi wa Shirika la Bandari ulisema kwamba kazi za kuokoa meli ya Fatih kwa sasa imekamilika na iliyobaki ni kuiburura na kuiondoa katika eneo la bandari ya Malindi.


Wananchi wengi walioshuhudia kazi ya kuibua meli hiyo wamelitaka Shirika la Bandari kujizatiti na kutafuta zana za kisasa kukabiliana na majanga kama hayo. Viongozi mbali mbali waliotembelea eneo la bandari wakati wa ajali hiyo, wamelitaka Shirika la Bandari kujipanga kwa kutafuta zana za kisasa katika kukabiliana na majanga.


Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini(IGP), Said Mwema na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange, waliutaka uongozi wa shirika hilo kutafuta zana za kisasa kukabiliana na majanga kama ya kuzama kwa meli.


Meli ya Mv.Fatih ilizama wakati ikitia nanga katika bandari ya Malindi, ambapo wati sita walifariki dunia. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imeunda tume kuchunguza chanzo cha ajali hiyo, huku taarifa za awali zikionyesha kwamba meli hiyo iliingiza maji sehemu ya mbele na kuzama wakati ilipokaribia bandari ya Malindi.

Chanzo: Gazeti la Uhuru

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.