Habari za Punde

MAMA SHADYA AHIMIZA IBADA,UPENDO KWA YATIMA

Na Mwanajuma Abdi TSJ
MKE wa Rais wa Zanzibar, Mama Shadya Karume, amewaasa waumini wa dini ya Kiislamu kusaidiana na kuongeza kufanya ibada kwa kufunga, kusoma Quraan pamoja na kutoa sadaka kwa wingi katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Hayo ameyasema juzi,katika hafla ya kuwafutarisha watoto yatima iliyoandaliwa na Vodacom Foundation huko katika Hoteli ya Bwawani mjini hapa, ambapo alisisitiza umuhimu wa kusaidiana na kupendana katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Katika hafla hiyo, Mkuu wa Vodacom Foundation Mwamvita Makamba, alimkabidhi Mama Shadya Karume zawadi za vifaa vya skuli madaftari na vyakula vikiwemo mchele, unga wa ngano, sukari, mafuta ya kupikia kwa ajili ya watoto hao.

Alisema ibada ya funga inawajenga watu kuwa na imani na kuacha kutenda maovu, ambapo inasaidia kujua ufalme wa Mwenyezi Mungu.
"Funga ni moja kati ya nguzo tano za dini yetu, ina manufaa makubwa sana kwetu, humshajihisha mtu kutenda mema na kuacha maovu, ambapo wataalamu wanatueleza kwamba funga nia jambo jema katika afya ya mwanaadamu, hivyo tujitahidi kutekeleza ibada hii kwa kadiri ya uwezo wetu na Mwenyezi Mungu atatulipa mema Inshaallah", alisisitiza Mama Shadya.
Aidha, aliusia jamii kuwapenda watoto hasa yatima, kwani kufanya hivyo Allah (S,W) atawateremshia neema nyingi hapa duniani na kesho akhera.

Mama Shadya ameushukuru uongozi wa Vodacom Tanzania na Vodacom Foundation kwa uamuzi huo wa kuwafutarisha watoto hao, ambapo alisema kitendo hicho ni kutekeleza nguzo moja muhimu ya dini ya Kiislamu.Hata hivyo, amezipongeza Taasisi mbali mbali ikiwemo Mfuko huo, kwa kuwasaidia watu wanaoishi katika mazingira magumu.

"Napenda kusisitiza kwamba msichoke kutoa ushirikiano wenu kila inapowezekana, muwe wabunifu wa mikakati ya kuwawezesha vijana wetu kwa kuwasaidia kuwapa uwezo wa kuyakabili maisha yao na kuwa mstaari wa mbele katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya na maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI", alieleza.

Nae Mkuu wa Vodacom Foundation, Mwamvita Makamba alisema kampuni ya simu ya mkononi ya Vodacom ipo mstari wa mbele kusaidia katika nyanja za elimu, afya na kutunza mazingira ili yasiweze kuharibiwa.

Alieleza kwamba, wanatoa kila aina ya misaada kwa watu wanaoishi katika mazingira magumu, ambapo mwezi huu unazidisha kuonesha upendo na ukaribu na watu hao.Aidha alisema kitendo cha kuamua kuwafutarisha watoto yatima ni kuwajengea upendo na kuwaonesha kwamba wapo karibu nao.

Kaimu Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Wafku na Mali Amaana, Khalid Mohammed Mrisho, aliishukuri kampuni hiyo kwa msaada huo, ambapo alisisitiza kwamba, Mtume Muhammad (S.A.W), aliusia kuwa mwenye kuwatendea wema mayatima atakuwa naye peponi bega kwa bega kama vilivyo vidole viwili vilivyokuwa pamoja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.