Habari za Punde

HATUFUNDISHANI KULEA BALI TUSAIDIANE MALEZI

Na Ashura M Hamad
Nipo tena kwenye safu yako azizi ili kuokoa malezi yetu ya asili yaliyogubikwa na wigo wa utandawazi. Sipo hapa kufundisha kulea lakini nipo hapa kwa ajili ya kusaidiana malezi ili yawe kama yetu sisi tuliolelewa tukaleleka miaka arobaini na nne iliyopita.

Ulezi sasa umekuwa mtihani mkubwa wa wazazi kila mmoja anasikitika na lake rohoni, ukiona kwako kunaungua basi kwa mwenzio kunateketea, wimbo wa watoto wa siku hizi hawasikii kila kichochoro na kibwagizo chake na sisi tulikuwa watoto lakini tulisikia tuliyokanywa, hili kushushia pumzi.

Tatizo hili la watoto wa siku hizi limesababishwa na jinamizi gani?

Kwa kweli tunaweza kusema utandawazi umeharibu watoto na sisi wazazi, maana wigo wa kulea watoto kimagharibi na vile vile mapenzi ya dhati kwa watoto hata vichwa vyao vikakuwa na wakatambua kama wanapendwa ndio chanzo cha mmong’onyoko wa maadili yetu.. Yote hayo hayakatazwi lakini wahindi wanasema “aste aste” na kidogo mkaripie anapokosea na usiwape uhuru sana mwisho ndio hutupanda vichwani sisi wazazi wao na kutuona machizi ingawa kuwa huru ni moja ya haki za watoto.

Mzazi kumbuka “Samaki mkunje angali mbichi.” Ni wajibu wa kila mzazi au mlezi kuandaa ratiba nzuri kwa watoto wetu wangali wadogo, ratiba ambayo itamuongoza vizuri na hata atapopata akili atajua ni nini wajibu wake, ratiba tuipange muda wa kuamka asubuhi na nini atalazimika kufanya katika matayarisho ya kwenda skuli au chuoni, muda wa kurudi kwa wakati, usaidizi wa kazi za nyumbani, muda mchache wa kucheza kwa kujumuika na watoto wenziwe, pia michezo ipi ya kucheza maana watoto wengine hawajui michezo wao kwao wakitoka asubuhi mpaka umtafute kwa bakora wapi kaenda kucheza.

Ni vizuri kumfahamisha mtoto ni michezo ipi mizuri kwa watoto. Kutambua kurudi nyumbani kwa wakati, suala la usafi, ni vizuri mtoto baada ya laasiri kuwa safi na kumkataza kucheza michezo ya mbio kujipakaza mavumbi. Pia ni muda mzuri wa watoto kwenda kutembelea jamaa kwenda kuamkia, ikiwa hana ni muda muwafaka wa kupumzika na ni muda mzuri wa kuangalia televisheni hasa vipindi vinavyowahusu watoto. Ikifika magharibi ni muda wa kujitayarisha kwenda darsa au tuisheni kwa wanaokwenda na wasiokwenda pia ni muda mzuri kwa kudurusu masomo yao ya dini na dunia.

Na ni muda mzuri kwa sisi wazazi au walezi kufuatilia masomo ya watoto wetu na kuwahoji masuala mbali mbali ambayo tunahisi yataweza kusaidia sisi wazazi kufahamu mabadiliko mbali mbali ya watoto wetu. Na tuhakikishe mida ya watoto kulala ni mapema sio kuchanganyika na watu wazima au kutizama vipindi vya kijitu kizima. Hichi ni kipindi kizuri katika kuwatayarisha watoto wetu katika maisha bora ya baadae. Hapo ulezi utakuwa utakuwa shuwari tena mengine yakitokea ndio majaaliwa yake Muumba katika shani zake .

Muonekano wa sasa kwa watoto wetu ni ule humtambui akiwa asubuhi wala jioni, mitaani fujo na zogo, michezo haina wakati maalum, twende tu na wakilala wahoi hata ndoto zao huwasuta wakiwa usingizini.

Wazazi na walezi wenzangu tusaidiane kwa haya ili tuweze kuyarudisha maadili yetu ya asili na enzi za mababu zetu mtoto ni wetu sote tuwekane sana wanapokosea, ni kweli uchungu wa mwana aujuae mzazi lakini kuzaa si kupata, kupata majaaliwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.