Habari za Punde

MZULA AVITAKA VIKUNDI ULINZI SHIRIKISHI VIFUATE SHERIA.

Na Ramadhan Himid

MKUU wa Polisi Jamii Makao Makuu, Mrakibu wa Polisi Asha Juma Mzula amevitaka vikundi vya Ulinzi shirikishi Shehia za Miembeni na Kwaalinato kufanya kazi kwa kufuata sheria, ili kufikia malengo na azma ya kupunguza kero za uhalifu katika maeneo yao.

Mkuu huyo alisema hayo katika kikao cha Maafisa wa Polisi Jamii na Vikundi vya Ulinzi Shirikishi vya Shehia za Miembeni na Kwaalinato huko ukumbi wa Mesi ya Polisi Ziwani mjini hapa.

Alisema wananchi wa shehia hizo mbili wana shauku ya kupunguza kero za uhalifu, lakini jambo la kuzingatia kwao ni kufuata sheria kwani kuchukua sheria mikononi mwao ni kwenda kinyume na malengo ya polisi jamii.

Mrakibu huyo alikemea baadhi ya tabia ya wanavikundi hao kushutumiwa kujichukulia sheria mikononi mwao na badala ya pale wanapowakamata wahalifu kuwapeleka vituoni jambo ambalo linaleta malalamiko kwa wananchi.

Naye Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Mjini, Mrakibu wa Polisi Mkadamu Khamis Mkadamu, amewaomba wananchi hao wa Miembeni na kwa Alinato kufanya kazi kwa kujali mipaka ya kazi zao kwani Jeshi la Polisi halitamvumilia mtu atakayevunja sheria kwa kisingizio cha kuwa yeye ni mwanakikundi wa ulinzi shirikishi.

Kwa upande wao wananchi wa Miembeni walisema tangu kuanzishwa kwa vikundi vya ulinzi shirikishi kwa kiwango kikubwa wamefanikiwa kupunguza kero za uhalifu ila wameliomba jeshi la polisi kushirikiana kukabiliana na vitendo vya uchangudoa ambao ni kero kubwa kwa kizazi kilichopo na kizazi kijacho.

Wamesisitiza kwamba suala la uchangudoa lisipodhibitiwa katika Shehia ya Miembeni kuna hatari vijana wengi wakaambukizwa magonjwa ya ukimwi kwa vile machangudoa hao wengi wao hufanya ngono zembe jambo ambalo ni mtihani mkubwa kwa vizazi vijavyo.

Aidha wananchi hao wamesema kwamba watu wengi wanadhani kuwa uchangudoa ni jambo la kawaida ambalo halina athari yoyote lakini athari yake inaweza kujitokeza miaka ya mbele pale ambapo nyumba nyingi zinaweza kuwa tupu kutokana na kufa kwa ukimwi kwani machangudoa hao baadhi yao inasadikiwa kuwa ni waathirika na ndio maana wanajiuza kwa bei chini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.