Habari za Punde

WAZIRI HAROUN - FITINA MWIKO OFISINI



Na Mwanajuma Abdi

WAZIRI wa Kazi, Uwezashaji, Wananchi, Kiuchumi na Ushirika, Haroun Ali Suleiman amesema hatoruhusu majungu wala fitina kwa wafanyakazi katika kuwajibika kuiletea maendeleo nchi.

Kauli hiyo aliitoa jana, wakati akizungumza kwa mara ya kwanza na watendaji na wafanyakazi wa Wizara hiyo, huko Mwanakwerekwe, Wilaya ya Magharibi Unguja.

Aliwaeleza wafanyakazi hao kubwa ni kufanya kazi kwa kujiamini na kudumisha nidhamu kwa wakati wote na kufika kazini sio zaidi ya saa moja na nusu na kuondoka kwa muda uliowekwa, ambapo alihimiza suala ya fitina na majungu katika meza yake halina nafasi.

Alisema mtu yoyote anatakapokwenda kumpikia majungu au fitina mwenzake kwake atawakutanisha ili kukomesha tabia hiyo, ambayo haitosaidia kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Alifahamisha kuwa, suala la nidhamu, uadilifu na kujituma wakati wa kazi ni muhimu na kila mmoja kujua anachokifanya kwa lengo la kujenga uchumi wa Zanzibar kwa vile Wizara hiyo inahusika moja kwa moja na kuwawezesha wananchi pamoja na vikundi vya kukopa na kulipa (SACCOS) zinaingia humo katika kuondosha umasikini nchini.

Aidha alitoa wasiwasi kwa kuwaambia mlango upo wazi wasimuogope na wala wasisite wanapokuwa na matatizo kwenda kumuona hata liwe na binafsi anaweza kuwasaidia ushauri katika kulitatua.

Waziri Haroun aliwataka wafanyakazi na viongozi wa Wizara hiyo na Taasisi zake kufanya kazi kwa pamoja na kujituma, ambapo miaka mitano ikimalizika kupatikane mafanikio makubwa, sambamba na maslahi bora na kumaliziwa ujenzi wa jengo la Wizara ili kuwe na nafasi za kutosha.

Hata hivyo, aliwahamasisha wafanyakazi kujiendeleza kwa mafunzo ya muda mfupi na mrefu, ambapo aliwaahidi kuwasaidia upatikanaji wa fedha kwa vile anauzoefu na mashirikiano mazuri na Wizara ya Elimu.

Wakati huo huo Waziri Haroun alikabidhiwa Idara ya Vyama vya Ushirika na aliyekuwa Waziri wa kilimo, Mifugo na Mazingira, Burhan Saadat Haji, ambae alimkabidhi vitendea kazi.

Waziri Haroun alimshukuru na kumuahidi ataendelea kushirikiana naye katika ushauri kupitia taasisi hiyo kwa vile ni mzoefu.

Nae Waziri Mstaafu, Burhan alisema Idara ya Vyama vya Ushirika inahusisha na SACCOS, ambapo changamoto bado ni kubwa katika kuwafikia na kuwajengea uwezo ili waweze kukuza uchumi na kupunguza umasikini nchini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.