Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Kijamaa ya Vietnam zimeafikiana kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano wa kiuchumi na kijamii ikiwa ni juhudi za kukuza maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa mataifa yote mawili.
Makubaliano hayo yamefikiwa wakati wa mazungumzo kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa VietNam Mhe. Bui Thanh Son yaliyofanyika jijini Hanoi, Aprili 28, 2025.
Maeneo hayo mapya yaliyopewa kipaumbele katika ushirikiano mpya kati ya pande hizo mbili yametajwa kuwa ni uanzishwaji wa viwanda vya kuongeza thamani mazao ya kilimo ikiwemo korosho, matunda na mbogamboga, teknolojia ya habari na mawasiliano, biashara na uwekezaji, kuimarisha ushirikiano wa sekta binafsi,ulinzi na usalama, madini adimu, elimu na mafunzo.
Waziri Kombo katika mazungumzo hayo pamoja na masuala mengine ametilia mkazo kuhusu uwekezaji kwenye sekta ya kilimo na kubainisha kuwa miongoni mwa changamoto inayoikabili sekta hiyo ni upotevu holela wa mazao baada ya mavuno na ukosefu wa viwanda na ujuzi wa kuyaongezea mazao thamani. Ametumia fursa hiyo kuiomba Serikali ya VietNam kushawishi wawekezaji kuja nchini kuwekeza katika eneo hilo.
“Sekta ya kilimo bado uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania, tunatambua kuwa Vietnam mmepiga hatua kubwa katika kuongeza tija ya kilimo kupitia matumizi ya teknolojia na mbinu bora za kisasa, tunaamini tukishirikiana katika eneo hili kupitia uwekezaji na mafunzo, litakuwa na mchango mkubwa kwenye agenda yetu yakuendelea kuimarisha usalama wa chakula nchini na kuongeza kipato cha wakulima wetu” alisema Waziri Kombo.
Sekta nyingine ambayo VietNam imeitaja kwenye vipaumbele vyake na kuonesha nia ya kuwekeza hapa nchini ni ujenzi wa viwanda vidogo na vya kati, hatua inayolenga kuongeza thamani ya mazao mbalimbali ikiwemo pamba, korosho na kahawa ambayo pia yatasaidia kutengeneza fursa za ajira kwa vijana.
Kwa upande wake Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa VietNam Mhe. Bui Thanh Son amesema wanaitazama Tanzania kama mshirika wa kipekee na wa kimkakati barani Afrika hivyo wapo tayari kufungua ushirikiano katika maeneo yote ya kiuchumi yaliyowasilishwa kwa manufaa ya pande zote mbili.
Vietnam, ni miongoni mwa mataifa yanayokua haraka kiuchumi barani Asia, mathalani katika robo ya kwanza ya mwaka 2025, ilirekodi ukuaji wa Pato la Taifa (GDP) kwa asilimia 6.93 ikiwa ukuaji wa juu zaidi kwa robo ya kwanza ya mwaka tangu mwaka 2020.
Ukuaji huu ulichochewa na ongezeko la uzalishaji viwandani, maendeleo katika sekta ya kilimo, ongezeko la matumizi ya ndani na utalii.
Vilevile mauzo ya nje na uagizaji wa bidhaa uliongezaka na kufikia USD bilioni 202.52, ikiwa ni ongezeko la asilimia 13.7 ikilinganishwa na kipindi kama hicho (mwaka 2023/24) ambapo mauzo ya nje yaliongezeka kwa asilimia 10.6, huku uagizaji wa bidhaa ukiongezeka kwa asilimia 17.0.
Waziri Kombo yupo katika ziara ya kikazi nchini Vietnam, huku Mataifa hayo mawili yakifikisha miaka 60 ya Uhusiano wa kiplomasia tokea ulipoanzishwa Februari 14, 1964.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo akisalimiana na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Viet Nam Mhe. Bui Thanh Son walipokutana kwa mazungumzo jijini Hanoi, Aprili 28, 2025.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Viet Nam Mhe. Bui Thanh Son katika picha ya pamoja walipokutana kwa mazungumzo jijini Hanoi, Aprili 28, 2025.
No comments:
Post a Comment