Habari za Punde

ZANZIBAR HEROES YATOKA SARE 0-0 NA AMAVUBI YA RWANDA

Yasubiri matokeo ya Mchezo kati ya Sudan na Ivory Coast

Golikipa wa Rwanda akidaka mojawapo ya mashambulizi yaliolekezwa langoni kwake huku Sbari Ramadhan China "Mkongwe" akinyemelea
Golikipa wa Zanzibar Ali Mwadini akiliacha lango lake kuokoa hatari iliyoelekezwa golini kwake na wanyarwanda
Timu ya Taifa ya Zanzibar Heroes imejiweka katika wakati mgumu kujua kama itaendelea Robo fainali ya mchuano wa Cecafa au laa baada ya kutoka sare bila ya kufungana na Amavubi ya Rwanda katika mchezo uliofanyika katika uwanja wa Taifa.

Kwa matokeo haya, Rwanda tayari imefuzu Robo fainali kwa kuwa na pointi tano na Zanzibar yenye pointi nne kusubiri matokeo ya mchezo wa mwisho kati ya Sudan yenye pointi moja na Ivory coast yenye pointi tatu.

Wanyarwanda nusura waandike bao mapema dakika ya tano wakati Nadir Haroub Cannavaro alipozembea na mpira kumfikia Peter Kagabo ambae alijiandaa kufumua shuti kali ila Cannavaro aliuwahi mpira na kuokoa.

Golikipa wa Zanzibar Heroes Ali Mwadini alifanya kazi ya ziada kwa kuzuia mpira uliokuwa ukielkea wavuni uliopigwa na Mugiraneza.

Ni siku ambayo mshambuliaji wa Zanzibar Heroes Khamis Mcha hatoisahau baada ya kukosa bao la wazi katika dakika ya 76 ya mchezo akiwa yeye na nyavu na kupiga mpira nje.

Kwa ujumla Timu ya Zanzibar ilidorora katika kipindi cha kwanza lakini ilipata uhai kipindi cha pili na ilipeleka mashambulizi kadhaa langoni mwa Rwanda. Rwanda waliweza kuweka mpira kimiani dakika ya 71 lakini refa alilikataa kwa kuwa tayari mshambuliaji wa Rwanda alikuwa ameotea.

Kocha wa Zanzibar, Stewart Hall alitolewa nje kwa kadi nyekundu na Refa kutoka Uganda.

Kwa matokeo haya Zanzibar itategemea miujiza ya kuwa timu mbili bora zitakazoungana na washindi, washindi wa pili wa kila kundi ili kujua hatma yake kama itaendelea robo fainali. Kama Sudan na Ivory Coast zitatoka sare, au Sudan ikishinda nayo itafikisha pointi nne na itategemea magoli ya kufunga na kufungwa.  

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.