Niliwahi kuandika huko nyuma kwamba kitendo cha Wajumbe wa ZFA kuchagua viongozi ambao hawaendani na hali halisi ya mambo ni kituko cha kufungia mwaka. Ila kituko hiki sasa kimegeuka kuwa kioja si kituko tena. Kwani uchaguzi ulitenguliwa kwa kukatiwa rufaa baadhi ya taratibu ilizojiwekea wenyewe ZFA kukiukwa huku kamati ya kusimamia uchaguzi ilishindwa kubaini dosari hizo.
Si hivyo tu ila maagizo yaliyotolewa na kamati ya kusimamia uchaguzi kwamba urudiwe katika muda wa wiki mbili umezidi kuichemsha ZFA na katibu wake Mzee Zam Ali kutamka hadharani mbele ya waandishi kwamba hilo haliwezekani kwani ZFA haina tena pesa za kufanya uchaguzi mwengine labda wapate mfadhili.
Kioja hiki kinazidi kuchekesha kwani hii kamati iliyosimamia uchaguzi ndio ilioutengua baada ya kushtuliwa na mrufaani ambae alikuwa mgombea uenyekiti.
Tunashukuru ingawa kesi ya nyani alipelekewa ngedere lakini alichukua uamuzi ambao umezidi kuwaweka mashakani viongozi waandamizi wa ZFA na kwa ujumla maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu ambao ni kipenzi namba moja visiwani.
Alaa kumbe mambo yenyewe ndivyo yalivyo kwa mgombea mmoja kukatwa jina lake kwa kushindwa kuwasilisha cheti cha kidatu cha nne na mwengine anapitishwa kwa kauli yake tu na ushahidi wa kiapo cha mahakama kwamba anacho. Hii ni kamati ya uchaguzi iliyoridhishwa na “vielelezo” na ikaridhika. Kama si harufu ya rushwa sijui ni kitu gani chengine.
Wajumbe wengine wa ZFA walihakikisha wanakuwepo kupiga “kura” na huku wakijijua kwamba hawana sifa hiyo ila kwa sababu ya malengo waliyohakikisha wanakuwepo. Na kura walipiga na kumchagua waliemchagua. Huku wenyewe hawajafanya uchaguzi miaka dahari.
Hiki ndiyo chama chetu tunachokitarajia kupeleka mbele mchezo wa kandanda uliokufa kama alfola umebakia mafupa tu. Chenyewe hakijijui hakijitambui na wala hakielewi kanuni zake.
Hawa wajumbe 52 waliokuwa na sifa za kuingia katika uchaguzi wa viongozi wa ZFA ndio wa kuwatafuta na kuwajua ni kwa mantiki gani wanapiga kura.Wanaangalia vigezo gani wakati wa kupiga na je wanaogombania hupewa muda wa kujieleza na kuhojiwa?
Kitendo cha kumualika Waziri wa michezo kwenye uchaguzi ule ni kitendo cha kuiaibisha ZFA yenyewe pamoja na kumuaibisha Waziri ambae alikuwepo kuiwakilisha Serikali. Na mpaka hii leo hatujasikia msimamo wa ZFA katika suala zima la sakata la uchaguzi au angalau kuwaeleza wananchi hasa kilichokuwepo nyuma ya pazia na hawakutaka wengine kukijua.
Basi mpaka Waziri siku ile mlimrushia changa la macho akijua kinachofanyika pale ulikuwa uchaguzi kumbe ulikuwa ni unyakuzi wa madaraka kwa walafi wachache. Chonde chonde jamani muombeni radhi Mheshimiwa Waziri kwani uchaguzi ule ambao ni ZFA pekee ndio waliojua undani wake na malengo yake umemdhalilisha Waziri kwani walitumia ugeni wake kubariki unyakuzi haramu wa madaraka.
Maandishi ya blog yako pamoja na 'background' vinaumiza macho!!!
ReplyDelete