Habari za Punde

AJALI ZA BARABARANI ZAUA 112 MWAKA 2010

Na Halima Abdalla

AJALI 685 za barabarani zimetokea Zanzibar na watu 112 kupoteza maisha, kutokana na ajali hizo kwa mwaka 2010.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa usalama Barabarani Kanda ya Zanzibar, Kamishna Msaidizi Muandamizi wa Polisi Makame Ali Makame ,alipokuwa akizungumza na Zanzibar Leo Ofisini kwake Malindi Mjini Zanzibar.

Alisema idadi hiyo ya watu waliofariki ni kubwa ikilinganishwa na ya mwaka uliotangulia. Kati ya hao wanaume 91 na wanawake 21.

Aidha, alisema kwa mwaka 2009 matukio ya ajali za barabarani yaliongoza kufikia 834 na kwa kuhusisha vyombo mbali mbali vya usafiri.

Alisema katika ajali hizo watu 98 walipoteza maisha yao wakiwemo wanaume 77 na wanawake 21 ambapo waliojeruhiwa walikuwa 889 wakiwemo wanaume 699 na wanawake 190.

Alisema katika kukabiliana na ongezeko la ajali, kikosi cha usalama barabarani kikishirikiana na Taasisi mbali mbali ikiwemo Idara ya usafiri,ZRB,Bima,JUMADU ,zilisaidia katika kupunguza makosa ya barabarani kwa kufanya operesheni mbali mbali za kukagua magari, kuchunguza uhalali wa leseni za madereva.

Sambamba na hayo alisema kikosi cha usalama Barabarani kwa kushirikiana na Mamlaka husika kwa mwaka uliopita kiliweza kuwafungia leseni madereva 18 kati yao 5 wamefungiwa mwaka mmoja na 13 wamefungiwa miezi miwili kila mmoja.

Sambamba na hayo alisema kwa mwaka huu kikosi cha Usalama Barabarani kitajitahidi zaidi kupunguza ajali pamoja na madhara yake ambapo lengo hili litaweza kufikiwa ikiwa sote kwa pamoja tutashirikiana

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.