Habari za Punde

SERIKALI YATAFUTA WATAALAMU KUJUA CHANZO CHA MIRIPUKO - BALOZI SEIF

Na Mwantanga Ame

SERIKALI imesema itatafuta timu ya wataalamu kutoka nje na ndani ya nchi ili kufanya uchunguzi wa kina kuhusiana na miripuko ya mabomu iliyotokea katika kambi ya Jeshi ya Gongo la Mboto mapema wiki hii.

Tamko hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais Balolozi Seif Ali Iddi, wakati akizungumza na waandishi wa Habari alipofanya ziara fupi ya kuwafariji wahanga wa tukio hilo katika Hospitali ya rufaa ya Muhimbili.

Balozi Iddi, alifika katika hospitali hiyo jana asubuhi baada ya kukagua eneo la kambi iliyosababisha kutokea kwa miripuko ya mabomu na siaha silizohifadhiwa katika maghala maalum katika kambi hiyo.

Akiwa katika kambi hiyo Balozi Iddi pamoja na Mkuu wa majeshi ya Ulinzi Tanzania Davis Aden Mwamnyange na Waziri wa Ulinzi Dk Hussen Mwinyi, aliweza kushuhudia kuwapo kwa uharibifu mkubwa wa tukio hilo pamoja vipande vya mabomu ambayo vilipatikana kutoka mitani.

Akitoa maelezo yake baada ya ziara hiyo alisema serikali imesikitishwa sana na tukio hilo kujitokeza tena na inakusudia kuunda timu ya wataalamu kutoka nje ya nchi na ndani ili kufanya uchunguzi wa kina tukio hilo

Alisema serikali imeshtushwa kutokea tena kwa matatizo hayo kutokana na hapo awali ilishayafanyia ukaguzi maghala yake na wakaguzi wa kimataifa na kuyapasisha kuwa yapo katika hali ya usalama.

Alisema kuwa sio kweli kama serikali imeshindwa kufanya uchunguzi wa kina baada ya matukio ya kambi ya mbagala kama inavyotangazwa na vyombo vya abari kwani ilishaita wataalamu na kueleza kuwa maghala ya Tanzania ya silaha yako katika kiwango cha kimataifa.

Alisema kuwa matukio yaliotokea yanaonekana yamekuja kwa bahati mbaya na serikali itahakikisha inafanya uchunguzi wa kina ili kufahau nini tatizo lililojitokeza.

Kutokana na matukio yaliojitokeza Balozi Iddi alisema serikali itahakikisha inagharamia taratibu za mazishi kwa watu waliofariki katika tukio hilo na majeruhi wanaoendelea kupata matibabu katika hospitali kuu ya Muhimbili.

Alisema matukio yaliotokea watanzania waone kuwa ni majanga yanayoweza kutokea wakati wowote na wasiyachukulie kama ni mambo ya kisiasa.

Alisema jambo la msingi ambalo Jeshi la wananchi itahitaji kulifanya kwa wakati huu ni kuona inaendelea kuwatoa hofu wananchi ili wahamasike kurudi katika majumba yao kutokana na hali ya usalama hivi sasa ipo shwari kutokana na kudhibitiwa kwa mabomu hayo.

Kuhusu suala hilo kuwa ni lenye kujirejea na serikali kudaiwa kushindwa kujiandaa nalo alisema sio kweli kwani tukio la mbagala liliweza kuhusisha na watendaji wa Jeshi hilo na kufariki lakini la gongo la mboto watendaji waliweza kujihami na kufanya madhara yake kutokuwa makubwa.

Alisema kuwa jambo la msingi hivi sasa linalohitajika kuandaliwa ni namna ya kuwarudisha wahanga wa matukio hayo waliopo uwanja wa Uhuru kwani kuwapo kwao katika eneo hilo wanaweza kupata matatizo kutokana na kuwa tayari baadhi ya vibaka wameanza kuvamia eneo hilo na kuwaibia.

Wakati akiwatembelea majeruhi hao aiwataka kuwa pole na serikali imo katika hali ya majonzi ya matukio hayo na kuwahakikishia kuwaangalia zaidi.

Mapema msemaji wa tukio hilo katika kambi ya Jeshi ya Gongongo la mboto, Aloyce Mwanjilile, alisema kuwa hadi jana asubuhi watu waliofariki kutokana na tukio hilo ni 20 lakini huku kukiwa na taarifa za kuongezeka kwa mtu mmoja ambapo bado hawajathibitisha hilo.

Alisema majeruhi ambao walipatikana katika ajal hiyo walifikia zaidi ya 200 na hivi sasa wameongeza kasi ya kuyasaka mabomu hayo katika mitaa ya Pugu, Yombo vituka, Kwebe na Tabata kutokana na kuwapo kwa taarifa za kusambaa mabomu hayo.

Alisema hasara ambayo imepatikana katika tukio hilo ni kubwa kutokana na kuangamia kwa maghala 23 ya kambi hiyo yakiwa na silaha, mabomu na miripuko, magari mawili ya kutunzia silaha, magari mawili pamoja na gari moja ya kivita.

Hasara nyengine ambayo aliitaja ni ya kuungua kwa mabweni mawili ya wanaume na wanawake pamoja na nyumba za askari walioowa.

Mkuu wa Majeshi ya linzi Davis Mwamnyange, alimueleza Makamu huyo kuwa watahakikisha jeshi la Ulinzi linaimarisha usalama katika kambi zake ikiwa pamoja na kufanya uchunguzi wa kina wa tukio hilo.

Nae Dk Mziraiwa katika Hospitali ya Muhimbili alisema majeruhi walopatiwa matibabu katika hospitali hiyo walifikia 83 na wako katika hali nzuri ya matibabu.

Alisema kazi ya kutibu majeruhi hao serikali imeweza kufanikiwa kutokana na kutimiza wajibu wao wakiwa katika timu maalum ambapo aliahidi kuwa kazi hiyo wataiendeleza hadi watapona.

Hadi mchana wengi wa majeruhi hao walishuhudiwa kuanza kuwa katia hali ya unafuu huku baadhi yao wakiwa tayari wameshatambuliwa na familia zao.

Hata hivyo majeruhi wawili kati ya watatu katika matukio hayo walikuwa hawajapata fahamu na wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali hiyo na wengine hawajatambuliwa na familia zao.

Tukio la milipuko ya mabomu katika kambi ya Gongolamboto limetokea Febuari 16 majira ya saa2.15 za usiku ambapo Makamu wa pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi amelazimika kukatisha ziara yake kisiwani Pemba na kushiriki kikao cha Kamati ya usalama wa taifa ambacho kilifanyika chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungao wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete.

1 comment:

  1. Aibu gani hii? ivi serikali haina wataalamu wakujua hayo miaka 50 madarakani? kama hujui madhara ya mabomu na jinsi ya kuyatumia, kuyatunza na madhara yake kwanini ukayanunua? kichekesho cha mwaka!!

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.