Habari za Punde

MKURUGENZI MANISPAA AJERUHIWA KWA TINDI KALI

Ni tukio linalohusishwa na biashara Darajani

Watu wane wapigwa mapanga Kilimahewa

Na Halima Abdalla

MKURUGENZI wa Baraza la Manispaa ya Zanzibar, Rashid Ali Juma (45) amejuruhiwa vibaya sehemu za usoni, kifuani, mapajani na sehemu nyengine baada ya kumwagiwa maji maji yanayoaminika kuwa ni tindikali na watu wasiofahamika.

Akithibisha tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Aziz Juma Muhammed, alisema mkasa huo ulitokea majira ya saa 2:45 usiku wa Alkhamis, karibu na nyumbani kwake.

Imefahamika kwamba Rashid alipatikana na kadhia hiyo muda mfupi baada ya kumaliza kusali sala ya Ishaa katika msikiti wa Amani, mita chache kutoka makaazi yake.

Kwa mujibu wa habari hizo, Mkurugenzi huyo huwa na kawaida ya kuzungumza baada ya kumaliza sala na waumini wenzake katika eneo karibu na msikiti huo.

Kamanda Aziz, alisema baada ya kutoka nje ya msikiti akiwa na wenzake alijitokeza kijana mmoja aliyekuwa amevaa jaketi na kummwagia maji yanayosaidikiwa kuwa ni tindikali na kupata majeraha makubwa na kuonesha washambuliaji hao walimkusudia yeye kwa vile hakuna mtu mwengine aliyepata majeraha yoyote.

Rashid alikimbizwa hospitali ambako hadi jana asubuhi alikuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mnazimmoja alikolazwa.

Kamanda Aziz alieleza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na upelelezi ili kuwabaini na kuwakamata wahusika wa shambulio hilo.

Hata hivyo, Kamanda alisema Jeshi la Polisi halijapokea taarifa ya kupigwa kwa Meya wa Baraza la Manispaa Zanzibar, Khatib Abdulrahman.

Baada ya kuwepo uvumi kwamba yeyey pia alishambuliwa kwa kupigwa, ingawa hakuna sababu za wazi zilizotajwa kuhusiana na shambulio hilo lakini inawezekana limehusishwa na uamuzi wa serikali wa kuzuia wafanyabiashara wenye makontena hapo Darajani.

Serikali kupitia Baraza la Manispaa limeamuru wafanyabiashara wenye makontena hapo Darajani kuhama mara moja na makontena yao yaondolewe, hatua ambayo wafanyabiashara hao wamekuwa wakiilalamikia.

Hatua ya kuyaondoa makontena hayo ilisimama kwa muda baada ya wafanyabiashara kufungua pingamizi mahakama kuu. Hata hivyo habari ambazo hazijathibitishwa zinasema serikali imeshinda na pingamizi hilo kutupwa.

Wakati huo huo, watu watatu wameshambuliwa vibaya na watu wasiojulikana katika eneo la Kilimahewa kwa kudhaniwa kuwa ni wezi kati ya hao mmoja alifariki dunia baada ya kufikishwa hospitali.

Kamanda alithibitisha tukio hilo ambalo alipata taarifa kutoka kwa wasamaria wema waliosema tukio hilo lilitokea karibu na Tawi la CCM Kilimahewa juzi alfajiri.

Kamanda huyo alimtaja aliyefariki kuwa ni Ali Nassor Muhammed (21) wa Kilimahewa ambaye alipata majeruhi ya kukatwa miguu ambaye alipofikishwa Hospitali ya Mnazi mmoja kwa matibabu majira ya saa 5:00 asubuhi alifariki Dunia.

Kamanda Aziz aliwataja wengine waliojeruhiwa kuwa ni Ame Silima Ame (18) wa Kilimahewa aliyepata majeraha sehemu mbali mbali za mwilini ikiwemo mikononi pamoja na kupigwa kwa marungu na bakora mwilini.

Mwengine ni Ali Ramadhan Abdalla (17) wa Magogoni ambae amepata majeraha maeneo ya mikononi na miguu.

Kamanda huyo, alisema kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa majeruhi hao watu hao walivamiwa kwa kudhaniwa ni wezi na kundi la watu wapatao 10 katika Tawi la CCM Kilimahewa.Alisema Jeshi la Polisi lilipofanya uchunguzi katika eneo hilo hakukuwa na aliyelalamika kuibiwa.

Alifahamisha kuwa majeruhi wote walichukuliwa na kufikishwa hospitali ya Mnazimmoja kwa ajili ya matibabu.Kamanda alisema mpaka sasa hakuna mtu aliyekamatwa kuhusika na tukio hilo na upelelezi unaendelea kubaini waliohusika.

Wakati huo huo Februari 12 Polisi waliokota mtoto mchanga wa siku mbili akiwa ametupwa huko Bububu akiwa hai.Alisema baada ya kuokotwa wasamaria wema walimfikisha Polisi na baadae kufikishwa hospitali ya Mnazimmoja kwa ajili ya huduma ya kwanza

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.