Tehran, Iran
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi amekutana kwa mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Dk. Mahmoud Ahmadinejad katika makazi ya Rais mjini Tehran.
Katika mazungumzo yao, viongozi hao wawili walikubaliana kuongeza ushirikiano kwa maslahi ya nchi hizo mbili pamoja na kuisaidia Zanzibar kuimarisha uchumi wake.
Balozi Seif ameelezea kufurahishwa kwake na safari yake nchini Iran na kusema amejifunza mengi ambayo Zanzibar inaweza kunufaika kutoka kwa ndugu zao Iran.
Alisema uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Zanzibar ni mzuri sana tokea zama za jadi na kuahidi kwamba serikali yake itauimarisha zaidi.
Alielezea matumaini yake kuwa uhusiano huo utaimarika zaidi hasa kwa kuwa Iran kama Zanzibar inafanana katika mambo mengi hasa utamaduni kwa kuwa mataifa yote yana idadi kubwa ya waumini wa dini ya Kiislamu.
Balozi Seif alitoa salamu zake za kheri na fanaka kutoka kwa wananchi wa Zanzibar kwa ndugu zao wa Iran katika sherehe za kuadhimisha sikukuu ya mwaka ya Nairuz.
Kwa upande wake Dk. Ahmadinejad alisema uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Zanzibar ni wa kihistoria na umejengeka katika misingi ya urafiki.
Alisema uhusiano na utamaduni wa pamoja wa nchi mbili utapelekea kupanuka ushirikiano wa karibu wa serikali za mataifa hayo mawili katika sekta mbali mbali za kiuchumi.
Rais Ahmadinejad alisema leo katika utamaduni wa Zanzibar na Iran nafasi ya heshima, urafiki, utakasifu na uadilifu ni ya juu sana na kubainisha kuwa masuala hayo ndiyo yanayohitajiwa na jamii katika dunia ya leo.
Aidha alisema sherehe za Nairuz ni Iddi ya mfungamano baina ya wanaadamu na kuongeza kuwa, Nairuz ni siku kuu ya kuwapenda wengine, kuondoa chuki na siku kuu hiyo ni ya mataifa yote duniani.
Alisema Iran iko tayari kuimarisha uhusiano na Zanzibar katika sekta zote za kiuchumi na maendeleo kwa maslahi ya wananchi wa Zanzibar.
Balozi Seif yuko mjini Tehran kushiriki sherehe za kimataifa za Nairuz. (habari na mtandao wa Irna).
No comments:
Post a Comment