Na Ismail Mwinyi
WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali,Ramadhan Abdalla Shabaan,amewataka wanafunzi wa Skuli ya Msingi Kijitoupele kuzidisha bidii katika masomo yao na kuachana na michezo isiyo na faida kwao.
Alisema wanafunzi hususan wa kiume hawanabudi wa kusoma kwa bidii na kuachana na vishawishi ambavyo havina faida na manufaa mazuri kwao kwani alisema kufanya hivyo kutawajengea misingi imara katika maisha yao ya baadae.
Waziri huyo aliyasema hayo katika hafla ya kuwazawadia wanafunzi waliofaulu kuingia mchipuo katika Skuli hiyo,ambapo alisema kwa matokeo yanaonesha wanafunzi wa kike ndio waliofaulu wengi kuliko wa kiume, hivyo nao hawanabudi kuzidisha juhudi ili nao waweze kuwa mbele katika mitihani yao ijayo.
Aidha Shaaban amewataka wazazi kushirikiana na walimu wa Skuli hiyo katika kuyatatua matatizo mbali mbali yanayoikabili Skuli ikiwemo kujenga uzio ambapo utasaidia kuondosha kero la kuingiliwa na wanyama ndani ya Skuli ili kuwajengea mustakbali mzuri vijana wao.
Hata hivyo alisema kutokana na wingi wa wanafunzi waliopo katika Skuli hiyo Wizara yake itashirikiana bega kwa bega na uongozi wa Skuli katika kukamilisha ujenzi wa Madarasa yaliyopo katika Skuli hiyo kwenye hatua ya uwezekaji.
"Kwa kuwa Skuli ina wanafunzi wengi kupita kiasi Wizara itatoa ushirikiano wa karibu katika hatua ya kuezeka ili msongamano wa wanafunzi uweze kupungua nafikiria wingi wa wanafunzi waliopo darasani inafikia 100 hivyo Serikali haina budi kutoa mchango wake ili kulitatua hilo,"alieleza.
Aliongeza kwa kusema kuwa kutokana na Skuli hiyo kuongeza madarasa ya Form 1 na Form 2 changamoto iliyopo kwa walimu juu ya usomeshaji hivyo aliwasihi kutoegemea upande mmoja kwani alisema kufanya hivyo kutawafanya wanafunzi wafeli katika mitihani yao.
"Ikiwa mmezidisha madarasa ambapo sasa mumeweka darasa la kumi hivyo msiegemee upande mmoja na kuwaacha darasa la saba bila ya kupata elimu inayostahiki kutawafanya waweze kufeli katika mitihani yao,"alisisitiza.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi,Mkuu wa wilaya ya Magharibi,Hassan Mussa Takrima,aliwapongeza wazazi wa wanafunzi hao kwa ushirikiano wa karibu waliouonesha kwa walimu wa Skuli hiyo katika kufuatilia maendeleo ya watoto wao ambapo alisema ni jambo zuri kwa wazazi kufanya hivyo.
Sherehe hizo za kuwazawadia zawadi wanafunzi waliofaulu kuingia mchipuo ziliandaliwa na uongozi wa Skuli hiyo ambapo jumla ya wanafunzi 22 walifaulu wakiwemo wanawake 15 na wanaume 7.
No comments:
Post a Comment