Habari za Punde

MAMA SHEIN AHIMIZA MALEZI YENYE MAADILI

Na Mwanajuma Abdi

MKE wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mama Mwanamwema Shein, ameitaka jamii irudi katika malezi yenye kufuata maadili ili kuondokana na matatizo mbali mbali yanayowakabili watoto katika miaka ya sasa.

Hayo aliyasema Mkurugenzi wa Wanawake na Watoto Rahma Ali Khamis, kwa niaba ya Mama Mwanamwema Shein, katika sherehe za Maulid ya kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W), yaliyoandaliwa na AL- Madrasatul Tan-Bihi L-Ghafilina ya Mbweni mjini hapa.

Alisema jamii inapaswa kuwalea watoto katika maadili mema ili kuwaepusha na matatizo mbali mbali yanayoibuka katika dunia, ambapo watoto wa kike na akinamama ndio waathirika zaidi.

Aidha alieleza kuwa ulezi unawahusisha baba na mama lakini cha kushangaza siku hizi akinababa wanawabaka watoto.

Aliongeza kusema hali hiyo imefikia kiwango kibaya kwani akinababa wanawabaka watoto, na hivyo kuwaweka pahala pagumu wazazi wa kike katika kukabiliana na ulezi.

Aliishauri jamii irudi katika mafundisho ya Mwenyezi Mungu katika kuwalea watoto ili waweze kufanikiwa katika maisha ya duniani na kesho akhera.

Aidha aliipongeza Madrasa hiyo kwa kupata mafanikio mbali mbali licha ya kukabiliwa na ufinyu wa nafasi, ambapo aliwahimiza washindane na vyuo vyengine kwa elimu na sio malumbano kwani Mwenyezi Mungu hapendi mifarakano katika dini ya kiislamu.

Mkurugenzi huyo, alisema maombi yao waliyoyatoa katika risala atayafikisha kwa Mama Mwanamwema Shein ikiwemo ombi la vyarahani kwa ajili ya kujikwamua na maisha.

Mengine ni kupatiwa mashine ya kipaza sauti, mabusati na mashine ya Fotokopi ili kwenda na wakati katika utoaji wa taaluma ya dini ya kiislamu.

Nae Mwanafunzi wa Madrasatul Tan- Bih akisoma risala alisema chuo hicho kilianza mwaka 1980, ambapo sasa kina wanafunzi 150.

Alisema kutokana na maendeleo makubwa yaliyofikiwa katika madrasa hiyo, sambamba na kwenda na mabadiliko ya kimaendeleo, inakabiliwa na matatizo ya mashine ya kipasa sauti, ufinyu wa nafasi na mabusati ya kukalia kwa vile imezidiwa na wingi wa wanafunzi.

Aliongeza kwamba, kutokana na mabadiliko ya mfumo wa kimaisha na kuomba wapatiwe msaada wa vyarahani na mikopo ili waweze kujisaidia kujikomboa na umasikini kwa vile wengine ni wakubwa na wapo hapo kwa ajili ya kuwaendeleza wenzao wadogo.

Katika maulidi hayo zilisomwa kasida mbali mbali na faslu kwa ajili ya kueleza sifa za Mwenyezi Mungu na Mtume Muhammad (S.A.W).

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.