Habari za Punde

SHAMBA LA MKURANGA LAIUMIZA KICHWA KAMATI

Na Mwantanga Ame

SHAMBA la serikali la Makurunge liliopo Bagamoyo mjini Dar es Salaam, limezidi kuwaumiza vichwa wajumbe wa Kamati ya Mifugo, Utalii, Uwezeshaji na Habari ya baraza la Wawakilishi baada ya kupokea taarifa kwamba sehemu ya shamba hilo limo mikononi mwa Halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo.

Hali hiyo imekuja wakati wajumbe wa Kamati hiyo walipokutana na wataalamu na watendaji wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi afisini kwao Darajani Mjini Zanzibar.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dk. Kassim Gharib Juma alisema bado suala hilo linaendelea kujadiliwa katika vikao kati ya afisi yake Tanzania Bara.

Katibu huyo alisema hali hiyo inakuja baada ya kamati ya wizara yake kujadiliana na taasisi husika kuhusu suala hilo lakini Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo imetoa hoja kudai kuwa eneo la shamba hilo limepangiwa mipango mbali mbali ya maendeleo.

Aidha alisema Halmashauri hiyo imedai kuwa eneo lililotolewa kwa ajili ya uzalishaji wa n’gombe jambo ambalo hivi sasa halipo.

Alisema wanachokiona hivi sasa ni kwa halmashauri hiyo kuweka vikwazo kulitoa shamba hilo ambalo tayari serikali kupitia Baraza la Mapinduzi lilishaagiza wizara iliopita ya Kilimo kukabidhi shamba hilo kwa Chuo cha Kilimo Kizimbani.

Majibu ya Katibu huyo yaliifanya sehemu kubwa ya wajumbe wa kamati hiyo kushikwa na kigugumizi na kuanza kuhoji masuala ambayo bado hayajapata majibu na kuwekwa kiporo hadi mwisho wa ziara hiyo.

Wakizungumzia maendeleo katika sekta hiyo Katibu huyo alisema wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kiasi kikubwa imeweza kufanikisha malengo ya serikali ingawa baadhi ya maeneo yamekuwa yakikumbwa na changamoto za kupatikana kwa bajeti ndogo.

Alisema miradi mbali mbali imeweza kufanyiwa kazi ikiwemo ya utoaji wa huduma za chanjo kwa wafugaji kwa kuwapa matibabu tafauti ya kichaa cha mbwa, kufunga uzazi wa mbwa, paka na kuendeleza mradi wa Usimamizi wa Mazingira ya Bahari na Ukanda wa Pwani (MACEMP).

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.