Habari za Punde

ZANTEL YAWANEEMESHA WAZANZIBARI

Na Khamis Mohammed

Washindi wawili wakabidhiwa gari,  wengine wane vespa

KAMPUNI ya simu za mikononi ya Zantel jana ilikabidhi zawadi mbalimbali kwa washindi wa promosheni ya ujumbe mfupi unaofahamika kama Hamisi ma SMS.

Washindi wawili walikabidhiwa gari ndogo maarufu aina ya suzuki huku wengine wanne wakivuna vespa, katika hafla iliyofanyika viwanja vya Muembekisonge mjini Zanzibar.

Akizungumza na Zanzibar Leo, Mkonde Makame (35), ambaye alishinda zawadi ya gari, alisema, kwa kiasi kikubwa amefaidika na promosheni hiyo na kuwataka wanachi wengine wa Zanzibar kuendelea kutumia huduma za Zantel.

"Sikufikiria kama siku moja nitamiliki gari, lakini Zantel imeniwesha kupata gari", alieleza, Mkonde, mkaazi wa Kwarara wilaya ya Magharibi mjini Unguja.

"Ilikuwa kama ndoto wakati nikipigiwa simu kuelezwa nimeshinda zawadi ya gari, lakini ilikuwa ndoto ya kweli".

"Kwa kiasi fulani sasa nitaweza kupambana na umasikini kwa vile gari hii nitaitumia kwa shughuli za kiuchumi".

Mkonde, alielezea, azma yake ya kuendelea kutumia mtandao wa Zantel huku akifaidika na promosheni mbalimbali zinazotolewa na kampuni hiyo.

Naye Salama Juma, mkaazi wa Nyerere wilaya ya Mjini, ambaye naye alijishindia zawadi ya gari, aliishukuru Zantel kwa kuanzisha promosheni hiyo yenye lengo la kuwajenga wateja wa Zantel.

Akizungumza katika hafla hiyo ilipambwa kwa mchezo wa mbio za mapikipiki, Mwezeshaji wa promosheni hiyo, Hamisi ma SMS, aliwashukuru wateja wa Zantel kwa ushirikiano wao na kampuni hiyo na kuahidi kuendelea kutoa fursa za promosheni mbalimbali kwa wateja wake.

“Sisi kama Zantel tunajivunia mafanikio tuliyoyapata kupitia promosheni hii na tunapenda kuwahakikishia wateja wetu kwamba tunatambua na kuthamini ushirikiano wao".

Promosheni ya Hamisi ma SMS imefanikiwa kuwafanya wateja wa Zantel kuwa mamilionea kutokana na kujinyakulia zawadi mbali mbali kupitia promosheni zinazoendeshwa na kampuni hiyo.

Kampuni ya Zantel ambayo imesajiliwa Zanzibar na kuchangia kwa kiasi kikubwa mapato ya serikali, imekuwa ikiendesha promosheni ya Hamisi ma SMS ikiwa na lengo la kuwatuza wateja wa Zantel kwa upendeleo wao na uaminifu kwa kampuni hiyo visiwani hapa na Tanzania kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.