Habari za Punde

JAJI MKUU ASTAAFU, AKISHAMBULIA CHAMA CHA WANASHERIA - ZLS

Kijakazi Abdalla,Zanzibar

HATIMAYE Jaji Mkuu wa Zanzibar, Hamid Mahmoud, anastaafu rasmi leo, huku akijigamba kuwa anaondoka akiwa kifua mbele na kukishambulia Chama cha Wanasheria Zanzibar.

Akizungumza katika sherehe za kuapishwa kwa mahakimu wapya wa ngazi ya wilaya na mikoa pamoja na Mrajis wa Mahakama Kuu, Jaji Mahmoud alisema “nastaafu kwa mujibu wa sheria na si kwa shinikizo.”Jaji huyo alisema Chama cha Wanasheria wa Zanzibar ni cha wababaishaji ambao hawazingatii weledi katika Tasnia ya sheria.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa Idara ya Mahakama visiwani Zanzibar, watu katika chama hicho wametawaliwa zaidi na jazba za siasa.”Hawa watu ni wababaishaji, wananionea choyo kwa sababu mtoto wangu, Fatma (jaji), kuteuliwa kushika wadhifa wa ujaji. Mimi nimemsomesha naomba na wao wasomeshe watoto wao,”alisema Jaji Hamid Mahmoud.

Jaji huyo mkuu, ametumikia nafasi hiyo kwa muda wa miaka 22 mfululizo.Katika hatua nyengine, Jaji Mahmoud alisema anakusudia kulishtaki gazeti la kila wiki litolewalo kwa lugha ya Kiswahili la Mwanahalisi, kwa kumchafulia jina lake.

Mbali na gazeti hilo, pia Jaji Mahmoud anakusudia kukifikisha mahakamani, Chama cha Wanasheria wa Zanzibar kwa madai ya kumchafulia jina lake.Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, inasisistiza kwamba Jaji wa Mahakama Kuu, ataendelea kushika wadhifa huo hadi kufikia umri wa miaka 60, ambapo anaweza kustaafu kwa hiari ama kuendelea hadi kufikia umri wa miaka 65 atakapostaafu rasmi.

Kifungu cha 95(3) cha katiba kinasema “Jaji Mkuu ataendelea kushika wadhifa huo mpaka pale atakapomaliza shughuli zote ambazo zilimfikia kabla ya kutimiza umri huo.”

Jumla ya mahakimu tisa waliapishwa jana na orodha yao inawajumuisha Khamis Ali Simai, Said Hemed Khalfan, Mbarouk Nassor Mbarouk, Ali Abrahman Ali na Omar Mcha Hamza.

Hali kadhalika, Valentina Andre Katema, Fatma Muhsin Omar, Rashid Machano na Sabra Ali Mohammed .

Pia Mrajis wa Mahakama Kuu, George Joseph Kazi.Hivi karibuni, Chama cha Wanansheria wa Zanzibar, kimekuwa kikimtaka Jaji mkuu huyo, kuachia ngazi kwa madai kwamba kuwapo kwake kulikiuka Katiba ya Zanzibar.

Chanzo -  Gazeti la Mwananchi 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.