SHIRIKA lisilokuwa la kiserikali linalojishughulisha na Malezi bora na afya ya uzazi (RFSU) lenye Makao yake makuu nchini Sweden limetoa msaada wa zaidi ya shilingi bilioni 1.6 kugharamia mradi wa afya ya uzazi na ujinsia unaotekelewa katika Halmashauri ya wilaya za Manyoni,Singida vijijini na Manispaa ya Singida
Kiasi hicho cha fedha kilichotolewa na shirika hilo zitatumika kwenye awamu ya kwanza ya mradi huo wa afya ya uzazi na ujinsia ulioanza rasmi mwaka jana na unatarajiwa kumalizika mwishonj mwa mwaka 2013.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa shirika lisilokuwa na kiserikali linalijishughulisha na masuala ya afya (HAPA) Mkoani Singida,Bwana David Mkanje kwenye ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu juu ya afya ya uzazi na ujinsia iliyowashirikisha waandishi wa Habari 17 wa Mkoa wa Singida.
Aidha mkurugenzi huyo aliweka bayana kwamba mafunzo hayo yanasimamiwa pamoja na kuratibiwa na shirika hilo la HAPA ambalo makao yake makuu yapo mjini Singida.Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo lengo kuu la mradi huo ni pamoja na kuimarisha ushiriki sawa wa wanaume katika masuala yote ya afya ya uzazi na ujinsia.
Hata hivyo Bwana Mkanje alisema pia kwamba mradi huo unalenga pia kupunguza vifo vya wanawake na watoto vitokanavyo na matatizo ya uzazi.Akizungumzia kuhusu semina hiyo ya waandishi wa Habari,mkurugenzi huyo aliweka bayana kuwa waandishi wa habari ni kundi mojawapo la wadau muhimu wa mradi huo na hivyo kutokana na taaluma yao watasaidia sana kuielimisha jamii juu ya dhana nzima ya mradi huo ilivyo.
"Tunatarajia waandishi wa habari watakuwa jukwaa letu la uhakika kufikisha ujumbe wetu kwa jamii bila kupotosha ili lengo letu liweze kutimia"alifafanua Mkanje.
Naye mwezeshaji wa semina hiyo,Bwana Cuthbert Maendaenda alisema baadhi ya wataalam wa fani mbalimbali nchini wakiwemo wa sekta ya afya,hawafanyi kwa vitendo shughuli walizozisomea na badala yake wanawaachia wasaidizi wao ambao hawajasomea kabisa fani hiyo.
"Kwa mfano waganga waliosomea masuala ya kuzalisha wanawake wajawazito hawawasaidii wanawake hao kujifungua salama,na badala yake wanawaachia wahudumu ambao hawajasomea kabisa kazi hiyo,wanafanya kazi hiyo kwa mazoea.”alisema Maendaenda.
“Ukiwauliza wale waliosomea sababu za kuacha kufanya shughuli hizo wao wenyewe,majibu yao huwa ni rahisi sana,utawasikia wanakwambia kuwa mshahara wanaolipwa haukidhi mahitaji",alisisitiza mwezeshaji huyo.
Kwa mujibu wa Bwana Maendaenda ambaye pia ni Meneja wa mradi wa Tanzania Men as Equal Partners (TMEP) tabia hiyo inachangia pamoja na mambo mengine ikiwemo vifo vya wanawake wajawazito pamoja na watoto.
Hata hivyo mwezeshaji huyo alisema upo ukiukwaji mkubwa wa haki ya faragha au usiri kwa wagonjwa wanaofanyiwa na baadhi ya wafanyakazi wa vituo vya afya.
Meneja huyo hata hivyo alisema kuwa ukiukwji huo unachangiwa na wagonjwa pamoja na jamii kwa kutokuzijua,kutozifahamu kwa kina haki zao mbalimbali za msingi, ikiwemo haki ya kutunziwa siri ya maradhi yanayomsumbua
No comments:
Post a Comment