Habari za Punde

MSALABA MWEKUNDU YATUMIA MILIONI 150 KUCHIMBA VISIMA PEMBA

Na Yussuf Hamad, Pemba

ZAIDI ya shilingi 150 milioni zimetumiwa na chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania (Red Cross), kwa ajili ya kuchimba visima 30 vya pampu za mkono katika katika Shehia na Vijiji mbali mbali wilaya nne za Pemba.

Akitoa taarifa za uchimbaji wa visima katika sherehe za kufunga mradi wa maji na Usafi wa mazingira huko Mfikiwa nje kidogo ya mji wa Chake Chake Kisiwani Pemba, msimamizi Mkuu wa mradi huo Mohammed Ali Saleh, alisema mradi huo uliochukuwa miaka mitatu na umewanufaisha zaidi ya wananchi 15,000.

Alisema mradi ulilenga kuondoa tatizo la maji katika maeneo ambayo huduma hiyo inapatikana kwa wananchi kuifuata umbali mrefu au haipatikani kabisa.

“Ili wananchi wachimbiwe kisima ni lazima waandike barua ya maombi kwa Red-Cross Pemba, na sisi baadae tunapeleka wataalamu wetu kwenda katika kijiji kuona hali halisi ya tatizo la maji tukiona lipo tatizo basi tunasaidia”alifafanua.

Mohammed, alisema mchango wa jamii katika kazi ya uchimbaji wa kisima ni nguvu kazi yao, na kuongeza kuwa hivyo imewafanya wajenge imani kwamba miradi hiyo ni yao.

Alifafanuwa kuwa kisima kimoja kimekuwa kikigharimu kati ya shilingi milioni tatu hadi milioni sita kulingana na ukubwa wa kisima kilivyo.

Alivitaja idadi ya visima hivyo vilivyochimbwa kuwa wilaya ya Mkoani visima 13, wilaya ya Chake Chake visima sita, wilaya ya Wete visima 7 na wilaya ya Micheweni visima sita.

“Visima vingi tumevichimba Shehia na Vijiji ambavyo maji ya bomba hayajafika, tumefanya hivyo ili kuwaepusha wananchi kuendelea kutumia maji yasio salama “alieleza.

Akizungumza katika Sherehe hizo, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Juma Kasim Tindwa, alisifu juhudi zinazochukuliwa na Red Cross katika kuwapatia wananchi maji safi na salama.

Alisema maji ni muhimu kawa maisha ya binadamu na viumbe wengine, hivyo juhudi hizo zinafaa kuendelezwa na wananchi wenyewe kwa kuvitunza visima hivyo ili viweze kutumika kwa kipindi kirefu kijacho.

“Nyinyi Red Cross sio tu mnawasaidia tu watu bali pia mmeunga mkono juhudi za Serikali, kwani Sera ya Serikali imetamka wazi kwamba kila mwananchi atapatiwa huduma ya maji safi na salama “alifafanua Tindwa.

Tindwa alisema Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za Red Cross, pale ambapo wanahitaji msaada wa Serikali kwa lengo la kuwawezesha kutoa huduma bora kwa wananchi.

Mapema katika risala yao wanachama wa Red Cross wa Mikoa miwili ya Pemba wameiomba Serikali kuwapatia nafasi za ajira pale panapotokea mahitaji Serikalini ili waweze kujikimu kimaisha kwani kazi wanazozifanya katika chama chao ni ya kujitolea.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.