Habari za Punde

WABADILISHA FEDHA TUNDUMA WAONYWA KUFANYA BIASHARA USIKU.


Na Issa Mwadangala.

Wafanyabiashara wa Mtaa wa Custam Mji wa Tunduma Wilaya ya Momba Mkoani Songwe, wanaojihusisha na kubadilisha fedha za kigeni, wamepewa elimu kuhusu madhara ya kufanya biashara hiyo nyakati za usiku sana au alfajiri ili kuepuka matapeli na wezi kutumia mwanya huo kuwaibia.

Elimu hiyo imetolewa Agosti 22, 2025 na Polisi Kata ya Kaloleni Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Sinai Mwaseba katika mtaa huo na kuwahimiza wafanyabiashara hao kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa kuhusu watu wasiofahamika au ambao si waaminifu, kwani kufanya hivyo kutasaidia kuimarisha ulinzi na kuepusha wimbi la utapeli dhidi ya wageni ili kulinda taswira ya biashara ya ubadilishaji fedha katika eneo hilo na Mji wa Tunduma kwa ujumla.

"Wekeni utaratibu wa kuwatambua wanaofanya shughuli mnayofanya kihalali, sambamba na kuchukua tahadhari ili kulinda fedha zenu ikiwa ni pamoja na kuepusha migogoro na wageni wanaotembelea eneo hili" alisema Mkaguzi Sinai.

Mwisho, Mkaguzi Sinai alihitimisha kwa kusema Jeshi la Polisi linaendelea kushirikiana na makundi mbalimbali ikiwa ni pamoja na wafanyabiashara katika kuhakikisha shughuli zao zinafanyika kwa usalama na kwa kufuata sheria.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.