Habari za Punde

KILA MMOJA AWAJIBIKE KULETA MAENDELEO NCHINI

KWA kipindi kirefu uchumi wa Zanzibar na watu wake umekuwa wa kusuasua moja ya sababu ikiwa ni kutowajibika kwa sehemu kubwa ya wananchi na viongozi.

Hali hiyo imesababisha pato la serikali na watu wake kuwa la chini, jambo ambalo linazorotesha uimarishaji wa huduma za jamii, ikiwemo miundombinu, afya, elimu na maji safi na salama.

Mbali ya kuwepo mzigo mkubwa kwa serikali ambayo ina upungufu wa fedha kwa kukusanya mapato kidogo, pia kuna wananchi ambao ni mzigo kwa wananchi wenzao kwa kutofanya kazi na kuwa tegemezi hali ya kuwa ni wazima na wenye nguvu.

Uhamiaji kutoka vijijini kwenda mijini Unguja na Pemba nao unaongezeka kila uchao, ikiwa ni wachache walio tayari kufanya kazi wakati wengi wakitegemea kulishwa na kuvishwa na wenyeji wao mijini bila aibu.

Kuna tabia ya vijana wetu wengi hapa nchini kuwa na tabia ya kuchagua kazi, halafu kuitupia lawama serikali kama hakuna kazi na ukosefu wa ajira umeongezeka, ilhali kuna kazi zinatafuta watu.

Wale waliosoma na wao wamekuwa na mawazo mgando kwamba ajira ni lazima upate serikalini, hali ya kuwa wana uwezo wa kuajiriwa kwenye sekta binafsi, pamoja na kuweza kujiajiri wenyewe kwa waliopata mafunzo ya ufundi na kazi za amali.

Mipango mbali mbali imebuniwa na Serikali katika kuwainua kimaisha wananchi kwa kuwawekea njia na mifuko maalum ya kuwapa mikopo ya muda mrefu na mfupi, iwapo watajikusanya katika vikundi na kuendesha miradi ya maendeleo.

Fursa hiyo nayo haitumiki vyema, kwani vijana wamekuwa nyuma mno katika kujikusanya na wengi wao kuabudu uzururaji na kutumia njia za mkato kupata fedha chap chap na wengi kuishia katika matendo maovu na wengine jela.

Wakati umefika wa wananchi wote kuwajibika kwa kuelewa kuwa maendeleo ya nchi yao yanategemea zaidi uwajibikaji wa mwananchi mmoja mmoja popote alipo na kwa kazi yoyote anayofanya.

Kwa wale tulioajiriwa na Serikali tusiichukulie kama sehemu ya uvivu, kwa vile mwisho wa mwezi tunapewa mishahara yetu ni lazima tuwajibike na wataoshindwa basi wawajibishwe.

Viongozi waliopewa dhamana za kuongoza taasisi za umma wawe mfano wa uwajibikaji, pamoja na kusimamia vyema majukumu yao na wanaowaongoza kwa kufuata sheria zilizowekwa na kuachana na ubinafsi au ubaguzi wa aina yoyote.

Kumekuwa na madai ya mara kwa mara ya wafanyakazi kutaka kuongezwa mshahara na malipo mengine, jambo ambalo ni sahihi kwa wale wenye kuwajibika pekee, kwani wengine hata hicho wanaholipwa si halali kwao kutokana na kutowajibika.

Tuna haki ya kuinyooshea vidole serikali pale inaposhindwa kutupatia haki zetu au kutekeleza wajibu wake, pale tu ambapo kila mmoja wetu amewajibika kutekeleza majukumu yake.

Tukielewa kuwa haki na wajibu ni watoto pacha, mafanikio ya utendaji wa serikali na nchi kwa jumla yanategemea uwajibikaji wa kila mmoja wetu, tekeleza wajibu wako upate haki yako.

Aidha tabia ya kuoneana haya katika kuwajibisha watendaji wazembe na wakorofi ni lazima iondoshwe na asiyewajibika, sheria za kazi zilizopo zifuatwe ili kumuwajibisha.

Hakuna kudharau kazi ya mtu mwengine, kwani mmoja wetu asipotekeleza jukumu lake, basi wale wanaojiona kuwa ni mabosi au wasomi, waelewe kuwa hawatoweza kufanya kazi zao.

Tubadilike kwa kuwajibika kujenga nchi yetu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.