Ataka watendaji wasikalie, wasibanie taarifa
Asema waandishi wafanywe marafiki, wasiogopwe
Na Mwantanga Ame
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amewataka viongozi na watendaji serikalini kuacha kuvibania taarifa vyombo vya habari na kuwakimbia waandishi wa habari.
Dk. Shein, alieleza hayo katika ukumbi wa Chuo cha Sayansi na Teknolojia Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar, ikiwa ni majumuisho kufuatia zaiara ya siku mbili aliyoifanya katika Mkoa wa mjini Magharibi.
Alisema si busara kwa watendaji kung’ang’ania kuzikalia habari na kuwanyima waandishi taarifa hizo, pamoja na kuwakimbia maofisini pale wanapofuatilia taarifa.
Alifahamisha kuwa ni lazima watendaji wa serikali kubadilika na kuhakikisha kuwa wanashirikiana kikamilifu na vya vyombo vya habari na kueleza maendeleo ya serikali badala ya kujenga tabia ya kuwakimbia.
Dk. Shein, aliwashangaa baadhi ya watendaji serikalini kushindwa kuvitumia vyombo vya habari kuelezea mafanikio yaliofikiwa katika utendaji wakati wakijua serikali ina mambo mengi ambayo wananchi wanahitaji kuyajua.
Alisema tabia ya kukimbia kuzungumza na vyombo vya habari juu ya mambo ya serikali inaweza kusababisha jamii kukosa taarifa za nchi yao na kuwepo mambo ya uongo kuenea katika jamii.
“Habari za uongo zipo nyingi, ipo siku nitasema wanatia chumvi maana hujasikika kujibu wanapokuwa hawana uhakika waje watuulize wakati wa propaganda za siasa umekwisha vyombo vya habari ni marafiki wa serikali, lazima wajenge uzalendo kwa wananchi wetu”, alisema Dk. Shein.
Aliwaagiza watendaji waifanye kazi ya kutoa habari kwani ndio njia pekee itayoweza kuisaidia jamii na wananchi kufahamu nini serikali yao inafanya katika kuwaletea maendeleo yao.
“Sasa serikali inataka kusema mambo yake, tutaunda utaratibu wa kutoa habari yoyote ya serikali, hatuna haja ya kuficha mchana wala asubuhi, tunajipanga kwani habari ni muhimu kwa maendeleo ya jamii”,alisema Dk. Shein.
Alisema mfumo wa sasa wa kuficha mambo umepitwa na wakati kutokana na ulimwengu kutumia teknohama kwa kupeleka mawasiliano katika jamii na sio kubakisha katika serikali pekee, ambapo serikali itatumia maofisa uhusiano kutoa taarifa za kila mwezi.
Dk. Shein, aliwataka watendaji hao kuacha kuviogopa vyombo vya habari kwa kuhofia kuandikwa sivyo wanavyotaka na badala yake watumie fursa hizo kwa kuelezea ukweli.
“Matumaini yangu tunawatumikia Wazanzibari, mengine yanayosemwa yaachane ya magezeti ukweli nitakwambieni mimi mwenyewe nitasema na nyinyi mtasema jipangeni kwa hilo” alisema Dk. Shein.
Dk Shein alisema wasilione suala hilo zito kwani hata pale serikali inapokosea basi wakubali kusemwa kwani hivyo ndivyo dunia inavyoenda na wanahitaji kuona wanabadilika kwa kuwafanya waandishi wa habari kuwa ni marafiki zao badala ya kuwakimbia.
Kikao hicho kiliwashirikisha watendaji wakuu wa serikali wakiwemo mawaziri, makatibu wakuu, wakurugenzi, na watendaji katika taasisi mbali mbali za serikali na vyama na serikali.
Kwa kawaida katika sehemu mbali mbali za utendaji kazi kunakuwa na waajiriwa maalum wenye jukumu la kutoa habari, watu hawa huitwa maafisa uhusiano au maafisa habari. Sasa tujiulize kwa hapa Zanzibar ni Wizara gani yenye watu wa aina hiyo? Ingawa hata kwa hizo taasisi chache zilizoajiri watumishi hawa hawashirikishwi katika masuala ya kiutendaji yanayowahusu na zaidi kwa kuonekana kuwa ushiriki wao utasababisha eti kuwa na maslahi yasiyowastahikia!!! Sasa katika hali kama hizi kamwe Mheshimiwa raisi asitegemee shughuli mbali mbali za kiutendaji serikalini kujulikana kwa wananchi na hata miongoni mwa wafanyakazi wenyewe. Angalia utendaji kazi katika serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na katika taasisi zilizoko huko zinavyochakarika kihabari, ingawa hata huko pia udhaifu mdogo mdogo upo kama alivyotanabahisha Mheshimiwa Kikwete katika semina elekezi ya hivi karibuni.
ReplyDeletePia Mheshimiwa Dr. Shein ajiulize kitengo cha habari cha Ikulu yake kina kazi gani? Hivi ni mara ngapi kimeshawahi kuratibu mikutano ya maafisa habari (kama wapo) then, ndio atoe lawama.