Habari za Punde

MFALME WA ASHANTI APONGEZA SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA

Ataka Afrika itatue migogoro yake wenyewe
Avutiwa utajiri wa kitalii Zanzibar

Na Abdi Shamnah, OMKR na Mwanajuma Abdi

MFALME wa Ashanti, Otumfuo Osei Tutu amesema Ghana na hususan Jimbo la Ashanti litaendeleza ushirikiano wake na Zanzibar kwa faida ya wananchi wake na kuainisha kuwa taratibu za kubadilishana uzoefu zinasaidia katika kukuza maendeleo.

Mfalme Tutu alieleza hayo kwa nyakati tafauti alipofanya mazungumzo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, alipokutana nao akiwa katika ziara ya siku moja Zanzibar.

Aliipongeza mageuzi ya kisiasa yaliyofanyika Zanzibar na kupelekea kuundwa kwa Serikali yenye mfumo wa umoja wa Kitaifa na kusema hatua hiyo ni upanuzi wa demokrasia.

Alisema muundo huo wa Serikali, umesaidia nchi kuwa na amani na utulivu, ambao unasaidia kuhamasisha wawekezaji kuja nchini hivyo kuongeza kasi ya maendeleo.

Aidha alitoa wito kwa Mataifa ya Afrika kukaa na kumaliza matataizo yao wenyewe bila ya kuwaita wageni kuja kuwatatulia.

Mfalme huyo alieleza kuvutiwa kwake na utajiri wa kitalii uliopo Zanzibar, baada ya kutembelea maeneo mbali mbali ya kitalii akiwa na ujumbe wake Zanzibar.

Miongoni mwa maeneo aliyotembelea ni Beit Aljaib Forodhani, hoteli za kitalii Kaskazini mwa Zanzibar na kuona shamba la viungo ikiwemo karafuu huko Kizimbani.

Mfalme huyo alisema uhusiano wa Tanzania, Zanzibar na Ghana ni  muda mrefu, hivyo ujio wake unazidisha kukuza ushirikiano huo.

Hata hivyo, aliwataka viongozi wa Afrika wajifunze na wasimamie ipasavyo maendeleo ya Bara hilo ili liweze kupiga hatua kubwa za kiuchumi kwa faida ya wananchi na mataifa kwa ujumla.

Akizungumza na Mfalme huyo ofisini kwake Migombani, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, ameiomba Ghana kupanua wigo wa ushirikiano kati yake na Zanzibar, na kuangalia uwezekano wa kuisaidia katika imarishaji wa kiwango cha elimu.

Alisema ushirikiano kati ya nchi mbili hizo ni wa muda mrefu, tangu wakati ule viongozi wa nchi hizo Hayati Abeid Karume, Mwalimu Nyerere na Kwame Nkrumah wakipigania Uhuru wa nchi zao na Afrika kwa jumla.

Alisema katika kuendeleza ushirikiano huo, kuna umuhimu mkubwa kwa Ghana ambayo imefikia maendeleo makubwa, kuisaidia Zanzibar katika kuinua kiwango cha elimu maskulini.

Alisema mbali na mipango madhubuti ya Serikali ya kuinua kiwango cha elimu ya msingi kupitia Teknolojia ya habari, Zanzibar inakabiliwa na changamoto kubwa ya upungufu wa walimu wa Sayansi kwa skuli za Sekondari.

Alieleza kuwa hali hiyo inatokana na wanafunzi wengi waingiapo sekondari kujikita katika masomo ya sanaa (art).

Aliitaka Ghana ambayo imepiga hatua kubwa katika sekta ya elimu kuangalia uwezekano wa kubadilishana uzoefu kwa walimu wake kuja Zanzibar kufundisha, ili kuimarisha fani ya sayansi.

Aidha alimuomba Mfalme huyo kuwashajiisha wawekezaji wa Ghana kuja kuwekeza katika sekta ya uvuvi wa bahari kuu, kwa maelezo kuwa kuna rasilimali nyingi ambazo bado hazijatumika ipasavyo.

Alisema uvuvi unaofanyika hivi sasa ni wa kienyeji, ambapo wavuvi huvua katika maeneo ya pwani, kutokana na ukosefu wa utaalamu na kuwa na vifaa duni vya kuvulia.

Vile vile Maalim Seif alitumia fursa hiyo kumuomba Mfalme Tutu kuangalia uwezekano wa kuisaidia Zanzibar katika dhamira zake za kuimarisha huduma bora za afya, akielezea changamoto kadhaa zinazoikabili sekta hiyo, ikiwemo upungufu wa madaktari, vifaa na wataalamu mbali mbali.

Maeneo mengine ambayo Maalim Seif aliomba kuendelezwa ushirikiano kati ya nchi mbili hizo ni pamoja na uimarishaji wa kilimo,hususan cha matunda na mbogamboga, akieleza azma ya wakulima wa Zanzibar kupata fursa ya kujifunza kutoka kwa ndugu zao wa Ghana.

Pia Maalim Seif alimweleza Mfalme huyo dhamira ya Serikali ya Zanzibar katika kuimarisha zao la Karafuu ili kuleta ushindani na nchi kadhaa duniani zinazozalisha zao hilo.

Alisema mbali na kuwepo uzalishaji mkubwa wa zao hilo kutoka nchi za Brazil, Indonesia, SriLanka na Madagascar, Serikali imejipanga vyema kuirejeshea  hadhi yake Zanzibar kama nchi inayoongoza kwa uzalishaji wa karafuu yenye ‘kiwango bora’ Duniani.

Alisema ili kufikia azma hiyo kuna umuhimu kwa Ghana kusaidia katika utafiti.

Katika hatua nyingine Maalim Seif ameiomba Ghana kusaidia utatuzi wa changamoto ya ugonjwa wa Ukimwi ili kupunguza na kuzuia maambukizo mapya sambamba na kukabiliana na uingiaji na matumizi ya dawa za kulevya, ikizingatiwa mazingira ya Zanzibar kuwa ni ya kisiwa.

Mapema akizungumza na Mfalme huyo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeweka kipaumbele sekta za kilimo cha umwagiliaji maji, elimu na kuimarisha huduma za afya katika kufikia maendeleo.

Mfalme Otumfuo aliwasili nchini asubuhi jana katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, ambapo alipokewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Mwinyihaji Makame, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Abdallah Mwinyi na viongozi mbali mbali wa Serikali.

Balozi Seif alimwambia mgeni huyo kuwa Zanzibar imepanga mikakati ya kuimarisha kilimo cha umwagiliaji maji ili kiwe mkombozi katika mapambano dhidi ya umasikini na kukuza uchumi.

Aidha alisema kitu chengine, kilichopewa nafasi ya juu katika mipango ya serikali ni kukuza elimu ya sayansi na teknolojia, itakayosaidia kuwa na wataalamu wa kutosha katika fani mbali mbali watakaosimamia afya bora nchini.

Balozi Seif alifahamisha kuwa, licha ya vipaumbele hivyo, huduma ya maji safi na salama itaimarishwa kwa vile Zanzibar inakabiliwa na changamoto kubwa ya uhaba wa maji na katika hilo, bajeti ya mwaka huu imetenga fedha maalum za kukabiliana na hali hiyo.

Alisema Zanzibar imeanzisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar ambayo imeamua kuwepo kwa muundo huo baada ya kumaliza uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, na kuridhiwa  na wananchi wote wa Zanzibar.

Aliongeza kwamba, muundo huo umejumuisha vyama viwili vikubwa vya kisiasa vya CCM na CUF kujumuika katika Serikali hiyo, ambayo inaongozwa na Rais wa Zanzibar kutoka chama cha Mapinduzi, Makamu wa kwanza Rais kutoka CUF na Makamu wa Pili wa Rais kutoka CCM.

Alisema muundo huo umesaidia kuleta amani na utulivu, jambo lililosaidia kufikiwa mikakati ya kiuchumi.

Aidha alimpongeza Mfalme Otumfuo kwa ujio wake  Zanzibar ambapo Ghana imekuwa na uhusiano wa muda mrefu tokea Rais wa Zanzibar wa Kwanza, Mzee Abeid Amani Karume, Rais wa Tanzania Julius Nyerere na Rais wa Ghana Dk. Kwame Nkrumah.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.