Habari za Punde

MIUNDOMBINU KUWEKA HUDUMA BORA UWANJA WA NDEGE, BANDARINI

Na Khamis Mohammed

WAZIRI wa Miundombinu na Mawasiliano, Hamad Masoud Hamad, amesema, wizara hiyo imeandaa mipango madhubuti itakayohakikisha kuwa inaimarisha huduma bora za sekta ya anga na bandari.


Hayo aliyaeleza wakati hafla fupi ya kukabidhiwa seti mbili za televisheni zinazotumia mawasiliano ya kisasa ya digital kwa ajili ya uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Amani Abeid Karume.

Alisema, kuimarika kwa huduma za katika maeneo hayo ya usafiri wa viwanja vya ndege na bandari kutaweza kuongeza idadi ya wasafiri na kuongeza pato la taifa.

Alisema, vifaa hivyo vitaweza kusaidia upatakanaji wa habari kutoka nchi mbalimbali kwa wasafiri wanaotumia uwanja huo sambamba na mawasiliano mengine ya kimataifa.

Waziri Masoud, alisema, wizara imejipanga vizuri katika kuyajengea mazingira mazuri maeneo hayo ili kuona yanatoa huduma za kisasa zaidi.

"Tumefanya mabadiliko ya kuanzisha mamlaka, chini ya mamlaka huduma zitaimarishwa ili kufikia lengo la utoaji huduma bora", alisisitiza, waziri huyo.
"Hali hiyo itaondosha kero mbalimbali katika viwanja vya ndege na kuzidi kuyavutia mashirika ya kimataifa kuleta ndege Zanzibar".

Mapema, Meneja Mahusiano na serikali, Charles Juta, alisema, Kampuni ya Simu ya Zantel itaendelea kushirikiana na serikali katika kusaidia maendeleo ya nchi na jamii kwa ujumla.

"Sisi Zantel tutaendelea kuwasaidia wanajamii katika kuhakikisha wanafaidika na kampuni yao katika huduma za kijamii", alisema, Juta.

Meneja huyo, alisema, lengo la Zantel ni kusaidia wananchi na wateja wake katika kuchangia maendeleo na kwamba siku zote itakuwa mstari wa mbele kutimiza malengo hayo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.