Habari za Punde

WAFANYABIASHARA KINYASINI WAIBEBESHA LAWAMA HALMASHAURI

 Na Mwantanga Ame

HALI imezidi kuwa mbaya katika soko kuu la Kinyasini linalotumiwa na wafanyabishara zaidi ya 50 baada ya kukosa huduma za matumizi bora ya vyoo huku biashara zinazouzwa sokoni hapo kutishia afya za wateja.


Hiyo ni kutokana na kuongezeka kwa ubovu wa vyoo katika soko hilo ambalo lipo tangu baada ya Mapinduzi ya Zanzibar 1964, limeshindwa kufanyiwa mabadiliko jambo ambalo limewafanya wafanyabiashara wa eneo hilo kuilalamikia halmashauri ya wilaya.

Wafanyabishara hao walieleza wanasikitishwa na hali hiyo, baada ya kuiona halmashauri ya wilaya hiyo ikiwa imejiweka pembeni katika kulifanyia mabadiliko soko hilo, huku ikiendeleza mlolongo wa kuweka ahadi zisizokwisha jambo ambalo limewakatisha tamaa.

Silima Juma, muasisi wa Soko hilo, aliiambia  Zanzibar Leo, wanalazimika kutoa lawama zao kwa halmashauri hiyo, baada ya kuona wameliweka kando suala la ujenzi wa soko hilo kwa muda mrefu licha ya kuendelea kutozwa kodi zinazotokana na biashara wanayoifanya katika soko hilo.

Fedha ambazo Silima alizitaja kwa ajili ya kulipia sehemu hizo alisema wamekuwa wakichangia shilingi 200 kwa siku ambapo kwa idadi iliyopo ya wafanyabiashra wa eneo hilo hufikia shilingi 25,000 kwa mwezi.

Michango hiyo alibainisha kuwa kama wangeliachiwa wafanyabiashara wa eneo hilo katika kipindi cha miaka miwili ama mitano wangeliweza kutumia fedha hizo kulifanyia mabadiliko soko hilo kwa vile hivi sasa lipo katika hali mbaya.

Alisema vyoo vya soko hilo, vina miundombinu mibaya baada ya kuchakaa ikiwa pamoja na kukosekana kwa huduma ya maji jambo ambalo husababisha kuwa na harufu mbaya ya vundo la mavumba ya samaki na matakataka yanayozalishwa katika sehemu hiyo.

“Hapa umekuja sasa hakuna mvua, lakini ikinyesha mvua hapa tunapishana na makambare matope chapwa chapwa utadhani tuko katika msimu wa kuvua tope”, alisema Mzee huyo.

Alisema hivi sasa wafanyabiashara wa eneo hilo wamekuwa wakijisaidia katika vichaka, jambo ambalo huwa ni baya pale inapotokezea mwanamke kushikwa na haja kutumia vichaka hivyo na huwalazimu kuwapatia msaada wa dharura katika nyumba za karibu na soko hilo ili wajisaidie wakati mwengine hukataliwa na wenye nyumba hizo.

Silima pia hakusita kubainisha kuwa katika soko hilo lenye uwezo wa kuwahudumia zaidi ya wakaazi 4,000 wanaoishi katika Mkoa wa Kaskazini na vijiji vya jirani kutoka kilomita 26 wa Mji wa Zanzibar, kuwa wamechoshwa na halmashauri yao kwa kulitelekeza huku wakiendelea kuchukua mapato yao.

Alieleza wanalazimika kuchoshwa na hali hiyo kutokana na hivi sasa hali ya utalii kukuwa katika vijiji vingi vya mkoa huo ambapo baadhi ya wawekezaji hulitumia soko hilo lakini inapotokea kunyesha mvua mapato yao hulazimika kushuka.

Kushuka huko kwa mapato yao Silima alieleza kunatokana na tabia ya baadhi ya wawekezaji hao kutopenda kujiingiza katika madimbwi ya maji machafu na hulazimika kubeba bidhaa zao kuzipeleka walipo jambo ambalo husababisha kutokea misokotano ya wenyewe kwa wenyewe katika kutafuta soko.

Hata hivyo alieleza kuwa uendeshaji wa huduma zao hivi sasa licha ya kukabiliwa na matatizo hayo lakini umekuwa ukienda vizuri kutokana na hapo awali kukabiliwa na matatizo ya kisiasa.

Akifafanua kauli hiyo alisema Soko hilo lenye asili ya wafanyabiashara wenye mitazamo tofauti ya kisiasa tangu hapo awali kutokana na kuwepo utengano wa kisiasa kabla ya Mapinduzi na kusababisha masoko hayo kuwa mawili yaliokuwa na misimamo ya vyama likiwemo la Chama cha Afro Shirazi Paty na Huzbulwatan.

Akizungumza juu ya suala hilo kwa sharti la kutotajwa jina mmoja wa maafisa wa Wilaya ya Kaskazini ‘A’ alisema tatizo kubwa ambalo limekuwa likichangiwa kuwapo kwa tatizo hilo ni kutokana na ukosefu wa kutambua namna ya uwajibikaji kwa baadhi ya viongozi wanaoziongoza halmashauri za Wilaya.

Alisema Uwajibikaji wa halmashauri ulitakiwa kuanza kwa madiwani waliopewa dhamana na wananchi kusimamia shughuli zao kwa kuwataka watendaji wa halmashauri kufanya usafi huku wakisimamia ukusanyaji wa mapato.

Alisema tatizo hilo linalojitokeza ni kwa watendaji hao kutoutilia manani uwajibikaji huo kwa kuona wapo zaidi kufanya shughuli za kutoa misaada kwa wananchi wa wadi zao, ikiwa ni hatua ya kujiweka sawa kisiasa.

“Diwani anaona ni vyema akatoe msaada katika Wadi yake ili aonekane kama anatimiza wajibu kuitumikia Wadi yake kama ilivyo kwa Mbunge na Mwakilishi lakini sio kuisaidia hii Halmashauri kuwa na mipango mizuri ya matumizi na kustawisha miji” alisema.

Miji kadhaa chanzo hicho cha Habari kilieleza kuwa imeonekana kustawi kutokana na halmashauri kufanya kazi zao vyema kupitia Mabaraza yao ya Madiwani kwani hulazimika kuweka hali nzuri katika masoko ili baadae waweze kukukusanya mapato vizuri.

“Tuangalie miaka mingapi hivi sasa tunatoa wafanyabishara kodi yao haibadiliki ni shilingi 200 tuu watendaji wa Halmashauri wanashindwa kuibadili kwa vile hawana jipya wanalolifanya katika masoko kwani yapo katika mazingira ya kizamani kabisa” Kilisema chanzo hicho. 

Kwa mujibu wa taarifa za halmashauri ya Wilaya ya Kaskazin ‘A’ iliyotolewa hivi karibuni katika kikao cha bajeti ya Wizara ya Nchi Afisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Ikulu, iliyosomwa na waziri wa wizara hiyo Dk. Mwinyihaji Makame Mwadin, alisema Halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2010/2011 ililenga kukusanya shilingi 50,milioni kutoka vyanzo mbali mbali vya mapato

Waziri huyo alisema hadi kufikia Mwezi Machi 2011 halmashauri hiyo imekusanya shilingi 62.7 milioni ikiwa ni sawa na asilimia 124 ya makadirio ya makusanyo ambapo kati ya hizo shilingi 28 milioni zimetumika kwa kazi za maendeleo na shilingi 24.6 milioni zimetumika kwa kazi za kawaida.

Aidha, waziri huyo alisema Baraza la Madiwani katika kipindi hicho liliidhinisha shilingi milioni 10, ambazo zilitumika kwa kutekeleza miradi ya ziada ukiwemo wa ujenzi wa barabara ndogo ya Pita na Zako hadi Kizimbani, Hospitali ya Kivunge na Skuli ya Chutama.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.