Habari za Punde

BALOZI AWATAKA WANAMSUMBIJI WAJITUME KIMAENDELEO

Na Haroub Hussein

WAZANZIBARI wenye asili ya Msumbiji wametakiwa kuungana na kujituma katika suala la maendeleo ili waweze kuondokana na umasikini uliopo ikiwa ni hatua ya kuwaenzi waasisi wa taifa lao katika kuwakomboa wananchi wao.


Kauli hiyo imetolewa na Balozi mdogo wa Msumbiji aliyepo Zanzibar, Bernardo Lidimba wakati akizungumza na wazanzibari na wanamsumbiji waliopo Zanzibar ikiwa ni katika hatua ya kuienzi siku ya mapambano ya Msumbiji sambamba na kumuenzi mwasisi wa Taifa hilo hayati Samora Moises Machel aliefariki kwa ajali ya ndege wakati akitoka Zambia kuelekea Msumbiji.

Balozi Lidimba alisema endapo wazanzibari hao wenye asili ya msumbiji wataungana pamoja katika suala la maendeleo kutawawezesha kupata faida mbali mbali zitakowapelekea kuondokana na suala la umaskini uliopo.

Aidha Lidimba alisema ni vyema wanamsumbiji wakajituma popote walipo bila ya kujali wapi wapo ila wazingatie kujituma na kuifanya Msumbiji kuendelea katika nyanja mbali mbali.aliwashauri wazanzibari hao wenye asili hiyo ya Msumbiji kutafuta elimu ambayo itawawezesha kuwafunza watoto wao masuala tafauti ya Nchi yao.

“Wanamsumbiji nakuombeni mjitume bila ya kuangalia wapi mlipo jambo la muhimu ni kujituma katika kuitafutia maendeleo Nchi yenu." alisema Balozi Lidimba.

Alisema Serikali ya Msumbiji imeamua kwa makusudi kuuweka mwaka 2011 kuwa ni mwaka wa kumuenzi hayati Samora Machel kwa kuzindua miradi mbali mbali ya maendeleo pamoja na kuweka minara ya kumbukumbu.

Lidimba alisema kwa upande wa Zanzibar wameanza shughuli mbali mbali za maendeleo ikiwemo kupanda miti katika maeneo tafauti, katika maeneo ya matemwe na dunga.

Aidha alisema Zanzibar kuna wazanzibari wengi wenye asili ya msumbiji ambao ni vyema nao kuwaanzishia mambo tafauti yatakayowafanya kwenda sambamba na utamaduni wa msumbiji.

“Katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar kama vile Tunguu, Bungi, Dunga,Ole,Chakechake na Wete kuna watu tafauti wenye asili ya msumbiji hivyo ndio maana tumeamua kuanzisha vitu mbali mbali vya utamaduni ili watu hao wasisahau utamaduni wao ikiwemo lugha." alisema Balozi huyo.

Aidha aliwataka wazee kuwapa elimu vijana wao ili vijana hao waweze kujikomboa kimaendeleo kwa vile elimu ndio msingi wa kila kitu.

Nae Mwenyekiti wa Jumuia ya Maendeleo ya Wanamsumbiji waliopo Zanzibar, Asilia Lunji alisema kuwa wazanzibari wenye asili ya msumbiji wanawajibu wa kujitahidi katika kuutunza utamaduni wa Taifa lao kwa lengo la kuwaachia msingi mzuri watoto wao ili wasije sahau utamaduni wa wazazi wao.

Ifikapo tarehe 19 mwezi Oktoba 2011 Msumbiji inatimiza miaka 25 tangu impoteze Mwasisi wake hayati Samora Moises Machel aliefariki kwa ajali ya ndege katika milima ya Mbuzini mpakani mwa Afrika ya kusini na Msumbiji.ambapo hadi sasa uchunguzi wa kifo hicho unaendelea.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.