NA NAFISA MADAI-MAELEZO ZANZIBAR
TANI 80 za mwani mkavu zilizokuwa tayari kusafirishwa kuelekea Unguja na gari aina ya Canter Mitsubishi inayobeba mzigo zimetumbukia katika gati ya bandari ya Mkoani Pemba.
Akizungumza mwandishi wa habari hizi Mkurugenzi Shirika la Bandari Pemba, Hamad Salim Hamad alisema gari hiyo ilitumbukia baharini ilipokuwa ikirudi nyumba kujiweka sawa tayari kushusha tani za mwani huo.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, alisema mwani huo ulikuwa unataka kupakiwa katika meli ya Mv. Jitihada tayari kuja Unguja na kusafirishwa nje ya nchi.
Alisema kuwepo kwa gari chini ya maji katika gati hiyo, imekuwa ikisababisha kuzuia meli yoyote kufunga gati hali ambayo inadhorotesha utendaji na kulitia hasara shirika hilo.
Hamad alisema gati ya Mkoani haina mashine ya kubebea vitu vizito ‘creen’, ambapo tagi ya shirika hilo kutoka Unguja imetumwa kwenda kuiopoa gari hiyo ili kuipa nafasi gati hiyo iendelee na shughuli zake kama kawaida.
“Hatuna budi kujitolea kugharamia uokoaji wa gari hiyo kwani kuwepo kwake kumekuwa kukidhorotesha shughuli za gati na kuifanya kupata hasara”,alisema Hamad.
Mkurugenzi huyo alifahamisha kuwa kutumbukia kwa gari hiyo kumetokana na makosa ya dereva aliyekuwa akiliendesha kwa kutokuwa muangalifu wakati akiirejesha nyumba.
Alisema marobota ya mwani huo mkavu yalinunuliwa na kampuni ya Sea Weeds, ambapo mara baada ya zoezi la uokoaji kukamilika shirika litakaa na kampuni hiyo ili kujadili hasara.
No comments:
Post a Comment