Habari za Punde

KASKAZINI 'A' WANAMUAMKO MDOGO KUFUATILIA MATUMIZI YA MIRADI

Ali Khamis (ZJMMC) na Simai Haji (TUDARCO)

WANANCHI wametakiwa kufuatilia matumizi ya miradi mbali mbali ya maendeleo inayotumia fedha za umma katika shehia zao ili kuepusha ubadhirifu wa fedha hizo.


Mwenyekiti wa jumuiya ya Zanzibar Current Generation Forum, Abushiri Said Khatib, alieleza hayo huko katika Chuo cha Elimu Amali Mkokotoni wilaya ya Kaskazini A, alipokuwa akiwasilisha ripoti ya utafiti juu ya matumizi ya miradi ya maendeleo kwenye wilaya hiyo.

Alisema kuwa lengo la utafiti huo ni kuangalia matumizi ya ujenzi wa miradi ya maendeleo yanayotumia fedha za umma katika sekta ya elimu na jinsi gani wanajamii wana uelewa juu ya miradi ya maendeleo iliyopo katika shehia zao.

Pamoja na hayo, alisema kuwa madhumuni ya kuwasilisha ripoti hiyo kwa wananchi wa shehia hizo ni kuwajenga wanajamii kuwa na tabia ya kufuatilia na kuuliza juu ya matumizi mbalimbali ya fedha ambazo zinatumika kwenye miradi ya maendeleo.

Akizitaja miongoni mwa shehia zilizofanyiwa utafiti, ni pamoja na shehia ya Kidoti, Potoa, Bandamaji, Kidombo, Kibeni, Pita na zako, Muange, Kigunda na Tazari.

Khatibu alisisitiza kuwa, uwajibikaji mzuri wa viongozi na wasimamizi wa miradi hiyo utapatikana endapo wananchi watajengeka na tabia ya kuuliza na kudadisi matumizi ya fedha.

Katika ripoti hiyo, alisema tafiti zinaonesha kwamba ushiriki wa wananchi katika miradi hiyo ni mdogo, jambo ambalo hupelekea matumizi makubwa ya fedha za umma kwani miradi mingi hupangiwa bajeti kubwa lakini hailingani na ujenzi husika kutokana na wananchi kukosa uelewa na kutokuwa na udadisi wa miradi.

Akizungumza kwa niaba ya masheha wa shehia hizo tisa, sheha wa shehia ya Kibeni, Mussa Makame Mussa, alisema kuwa wameipokea vyema elimu hiyo na watahakikisha wanaunda kamati maalum katika shehia zao hizo ili kufuatilia matumizi ya miradi mbalimbali ya maendeleo na kuondoa tatizo la uharibifu wa mali za umma.

Aidha sheha huyo alisema miradi mingi ya maendeleo haina wakaguzi na baadhi yao hufuatiliwa kwa hatua za mwanzo tu jambo ambalo hurejesha nyuma maendeleo ya miradi hiyo.

Mpango wa utafiti juu ya matumizi ya mali za umma katika miradi ya maendeleo ulianza Agosti 22 na kumalizika Agosti 28 mwaka huu, huku jumla ya watu 800 kutoka shehi ya tisa za wilaya ya Kaskazini 'A' wakiulizwa maswali juu ya ushiriki wao katika miradi mbalimbali ya maendeleo yanayotumia fedha za umma kwenye shehia hizo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.