Na Haroub Hussein
BENKI ya Diamond Trust (DTB) imesema itaendeleza mpango wake wa kusaidia jamii hasa watoto yatima na wazee wasiojiweza ikiwa ni mpango maalum wa kuirejesha sehemu ya faida inaypatikana na benki hiyo kwa jamii.
Meneja wa Benki hiyo kanda ya Zanzibar, Othman Juhudi aliyasema hayo kwa nyakati tafauti alipokuwa akikabidhi zawadi mbali mbali za sikukuu ya Eid el Fitri kwa watoto yatima walioko katika nyumba ya Mazizini na wazee wasiojiweza walioko Sebleni mjini hapa.
Juhudi alisema benki yake itaendelea kutoa misaada mbali mbali kwa jamii ikiwa ni hatua ya kuwaondolea matatizo yanayowakabili na kuwapatia mahitaji muhimu kila inapohitajika.
Alisema utaratibu huo watauendeleza katika sikukuu mbali mbali za kitaifa kwa kutoa michango tafauti ikiwemo fedha, chakula na huduma nyengine za kijamii, ambapo aliahidi kushirikiana na wanajamii katika kutoa misaada mbali mbali itakayowasaidia katika suala zima la kuondokana na umaskini.
"Benki yetu itaendeleza utaratibu wa kuisaidia jamii katika masuala mbali mbali ikiwa ni miongoni mwa mikakati yetu tuliojiwekea kutumia sehemu ya faida tunayopata kuirudisha kwa jamii ambao ndio wateja wetu",alisema meneja huyo.
Nae msaidizi mlezi katika nyumba ya kulelea watoto yatima Mazizini, Maryam Makame aliupongeza uongozi wa benki hiyo kwa uamuzi wao wa kuwapatia msaada huo uliokwenda sambamba na sikukuu ya Eid el Fitri.
Maryam aliitaka benki hiyo kuendelea kutoa misaada mbali mbali kila wanapopata uwezo wa kufanya hivyo na kuzitaka taasisi nyengine kuiga mfano wa benki ya DTB.
Kwa upande wake mdhamini wa nyumba za wazee Sebleni, Khamis Salum aliipongeza benki hiyokwa msaada wao ambapo alisema utaweza kuwasaidia hasa katika kipindi hiki cha skukuu ya iddi.
Alisema misaada hiyo itawapa faraja wazee wanaoishi katika nyumba hizo na kuahidi kuwa misaada hiyo itawafikia walengwa,na kuiomba benki hiyo kuendelea kutoa misaada kila inapopata wasaa wa kufanya hivyo.
Misaada hiyo iliyotolewa na DTB ni pamoja na michele, mafuta na mbuzi nyenye thamani zaidi ya milioni moja na nusu.
Jamani tisiishie kushukuru tuu, na wao tunawapa support kwa kufungua account kwenye Benki yao? au hatuelewi kuwa bila kufanya hivyo watafunga virago na kuondoka?
ReplyDelete