DAR ES SALAAM
MATUMAINI ya Watanzania leo, yataelekezwa kwa timu yao ya taifa ya soka 'Taifa Stars', inayoikaribisha 'Desert Warriors' ya Algeria katika mechi ya kundi 'D' kuwania tiketi ya fainali za mataifa ya Afrika mwakani.
Mpambano huo umepanwa kurindima mnamo saa 10:00 jioni ambapo Stars itakuwa ikisaka ushindi kwa udi na uvumba ili kujijengea mazingira mazuri ya kutinga fainali hizo kwa mara ya pili katika historia.
Fainali za mwakani zinatarajiwa kuandaliwa kwa pamoja na nchi za Gabon na Guinea ya Ikweta.
Kocha wa Taifa Stars Jan Poulsen, anatarajiwa kupanga wachezaji wote mahiri wakiwemo wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi, kwa lengo la kupata ushindi ambao ni muhimu ili kufufua matumaini ya Tanzania kutinga fainali hizo.
Miongoni mwa nyota hao ni Idrisa Rajab anayechezea Sofapaka ya Kenya, Mbwana Samatta na Mussa Mgosi wa DC Motema Pembe ya DRC, Henry Joseph na Abdi Kassim wanaokipiga nchini Vietnam.
Wachezaji wengine wa kikosi hicho ni Shabani Dihile, Juma Kaseja, Shabani Kado, Shadrack Nsajigwa, Amir Maftah Aggrey Morris, Juma Nyoso, Victor Costa, Nurdin Bakari, na Shabani Nditi.
Wengine ni Juma Seif, Jabir Aziz, Nizar Khalfan, Mrisho Ngasa, Abdi Kassim, Mbwana Samata, Ramadhan Chombo, Dan Mrwanda, Athuman Machupa and John Bocco.
Hata hivyo, kocha Poulsen amesema hataita mchezaji mwengine kujaza nafasi iliyoachwa na kiungo Salum Machaku aliyeondolewa baada ya kuumia kidole, bali atapanga mchezaji miongoni mwa walioko kambini.
Machaku amewekewa POP na anatarajiwa kuwa nje ya dimba kwa kipindi kisichopungua mwezi mmoja.
Timu ya Algeria iliyowasili nchini Alkhamisi usiku ikiwa na msafara wa watu 60, inajivunia nyota kadhaa wanaochezea ligi katika klabu mbalimbali za Ulaya, wakiwemo Nadir Belhadj, Karim Ziani na Hassan Yebda.
Mchezo huo utachezeshwa na waamuzi kutoka Mauritius ambao ni Ali Lemghaifry, Mohammed Hamada, Hassane el Dian na Pene Cheikh Mamadou, huku Nicholas Musonye kutoka Kenya akiwa kamisaa wa mechi.
Pambano jengine la kundi hilo, litazikutanisha Morocco na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Morocco ndiyo inayoongoza kundi hilo ikiwa na pointi saba sawa na Afrika ya Kati inayoshika nafasi ya pili nyuma ya Morocco kwa tafauti ya magoli, huku Stars ikiwa katika nafasi ya tatu baada ya kufikisha pointi nne, sawa na Algeria wanaoshika mkia pia kwa tafauti ya mabao
Hapatoshi nini, na wamekalizimishwa droo ya 1-1,nyumbani?
ReplyDelete