Habari za Punde

KONGAMANO LA WANAHABARI LAFANYIKA KUADHIMISHA SIKU YA TAARIFA DUNIANI

Meneja Mwendeshaji wa Baraza la Habari Zanzibar Chande Omar alikuwa mgeni rasmi katika kongamano lililofanyika katika ukumbi wa kituo cha elimu mbadala
Mwandishi na Mwanahabari mkongwe wa BBC Ally Saleh (Alberto) akiwasilisha mada yake kuonesha mafanikio na changamoto zilizopo kwa Baraza la Habari (Angalia chini ya Picha kwa ripoti kamili)
Baadhi ya Waandishi habari mbalimbali waliohudhuria,  viongozi wa Siasa na Wanasheria waliohudhuria kongamano hilo wakisikiliza kwa makini moja ya taarifa zilizokuwa zikitolewa.


Ally Saleh,

Leo Jumatano September 28 ni siku ya kimataifa ya kupata taarifa yaani International Day for the Right to Know ambayo itasherehekewa hapa nchini kwetu kama ambavyo inasherehekewa nchi nyengine nyingi duniani.

Hii ni sherehe muhimu kama vile waandishi wa habari wanavyoshererehekea siku ya uhuru wa vyombo vya habari au sherehe nyengine nyingi ambazo zinakumbusha juu ya demokrasia na uhuru katika upana wake.


Siku hii haikuanzishwa zamani sana na kwa hivyo haina historia refu. Inavyoonyesha ni kuwa kwa mara ya kwanza ilisherehekewa huko Sofia, Bulgaria mwaka 2002 ambapo mataifa yalikusanyika kutizama njia za kukuza mawasiliano duniani.

Hii hata hivyo maana kuwa siku hii haina mashiko kwa kuwa si ya zamani, la. Siku hii ina historia ndefu isiyo ya moja kwa moja kwa upya wake, lakini haki ya kujua imekuwa ikipiganiwa na mwanadamu tokea mwanzo wa maisha yake.

Kuna vipengele vingi katika matamko ya zama lakini pia kumekuwa na vipengele vingi katika katiba za wanadamu kwenye nchi zao na hayo yote ni ishara kuwa siku hii ni muhimu kwa maisha ya kila siku ya mwanadamu.

Ili binaadamu aishi ni lazima ajue, na ili aishi vyema zaidi ni lazima awe na haki kujua juu ya mambo ambayo yanazunguka maisha yake ya kila siku, maana uhai wake ni mnyororo unaotegemeana na kipingili kimoja cha mnyororo kikiwa na kasoro basin na yeye anakuwa na kasoro.

Hapana shaka haki ya kupata taarifa au haki ya kujua inatofautiana kati ya nchi na nchi. Kwa fikra zangu ni kuwa kila nchi ikiwa imeendelea zaidi basi tabaan haki ya kupata taarifa au haki ya kujua inakuwa pana zaidi.

Ila pia inawezekana hilo lisiwe kweli katika baadhi ya mambo ambapo kila nchi ikiwa imendelea na kwa hivyo uzalishaji ni mkubwa basi makampuni makubwa kama vile yanayohusika na masuala ya kemikali yanakuwa na siri nyingi zaidi za kuficha na hivyo yanakuwa makali yakitakiwa kutoa taarifa.

Kwa kuzingatia hilo ndipo mataifa yakaelekea katika kukubaliana kuwa kuna umuhimu wa kuwa na sheria inayotwa ya kupata taarifa yaaani Right to Information lakini wengine wakiita Freedom to Information.

Tanzania na Zanzibar hatujawa bado na sheria hii lakini kupitia Baraza la Habari la Tanzania (MCT) tayari kuna rasimu ya sheria hii ikiwa inaendelea kusota katika ngazi mbali mbali za kitendaji kabla ya kuona muangaza wa Bunge na Baraza la Wawakilishi.

Kwa hivyo mbali ya kuwa na sheria hii, lakini siku ya Septemba 28 itaendelea kuwepo kama ni siku ya kukumubushana kuwa haki ya kujua au kupata taarifa ipo ndani ya taifa na pia kuwa ni siku ya kupima na kujikosoa kwa tulioyafanya kuhusiana na haki hiyo.

Pamoja na ustaarabu wake mkubwa wa sheria na haki za binaadamu na uhuru wa kujieleza lakini Uingereza na Marekani hazikuwa nchi za mwanzo kuweka sheria ya haki ya kupata taarifa.

Nchi ya mwanzo ilikuwa ni Sweden katika mwaka 1766 tukijua pia kuwa Sweden hiyo hiyo ilikuwa mstari wa mbele kabisa katika uvumbuzi wa mashine za kuchapishia ambazo hivi sasa tunaziona ni jambo la kawaida tu.

Kinyume cha kuwa na sheria ya kupata habari ni kutandika sheria ya siri za serikali ambapo Uingereza ilikuwa ni moja ya nchi za mwanzo katika mwaka 1878 kutoka na mfanyakazi mmoja wa Serikali kushutumiwa kuvujisha siri za Serikali.

Mfanyakazi huyo Charles Marvin alichomoa kurasa chache kwenye madaftari ya Serikali na akanukuu vipengele katika mkataba baina ya Urusi na Uingereza na kuzipenyeza taarifa hizo kwa vyombo vya habari. Palikosekana vipengele vya kumshitaki na kwa hivyo akasalimika na hatia.

Lakini sote tunajua jinsi uwepo wa sheria ya siri za serikali unavyotumika vibaya na watawala na kwa hivyo kuwa ni njia mojawapo ya kuficha uchafu, uzembe na hata matumizi mabaya ya fedha na madaraka miongoni mwa watendaji na wakati mwengine kwa dhulma kubwa dhidi ya umma.

Kwa hivyo kuwepo kwa siku hii na uwepo wa sheria ya kupata taarifa kunatakiwa kurahisishe, kuratibu na kuwezeshe mwananchi kupata taarifa anayoitaka kutoka Serikalini ili akidhi haja, kiu au matarajio yake.

Inavyotakiwa kuwe na chombo kinachosimamia suala hilo na chombo hicho kiwe huru na taarifa ziwe zinatolewa kwa wakati unaofaa maana taarifa inayotolewa kwa wakati usio wake haiwezi kuwa na faida kwa mpokeaji au aliyeiomba.

Sina hakika nini kimo katika mapendekezo ya sheria za kupata habari zinazosukumwa na MCT lakini ningependa sana iwe imeundwa kwa kutizama muundo wa India ambayo mazingira yetu yanafanana zaidi lakini pia ni kwa kuwa India na wananchi wake wana mifano mizuri ya kuigwa katika kupigania haki zao, pamoja na umasikini na nguvu kubwa zilizo mikononi mwa mabepari.

Sheria ya India ya 2005 tayari ina mifano mizuri ya mafanikio kutokana na wananchi wa India kuichangamkia na hapa tunatoa mifano michache kuona hata mtu wa chini anawezaje kufaidika na uwepo wa sheria kama hii.

C.N. Kumar aliegesha gari yake sehemu na kulipishwa ada ya Rupia 10 badala ya Rupia 5 kitaratibu. Alipinga jambo hilo lakini haikumsaidia kitu. Kwa kutumia sheria ya kupata habari alipeleka masuala yake katika taasisi inayohusika na baada ya muda mkandarasi aliekuwa akisimamia maegesho hayo alipokonywa kandarasi hiyo.

Ramesh Phongade alikuwa ni mstaafu ambaye alistahili kulipwa Rupia 7,000 lakini akalipwa Rupia 5,000 na malalamiko ya miaka mine na panda shuka kadhaa na hata kufika kwenye Mahakama ya Pensheni na ndipo alipundua kuwepo kwenye sheria hiyo na haki yake ikapatikana na akaongezwa pensheni ikawa Rupia 8,000 na kulipwa pia usumbufu.

Vijay Kumbar yeye aliandika madai ya kutaka taarifa juu ya usambazaji mbaya wa gesi ambapo yeye na watu wengine walikuwa wakipata kiwango chini ya mahitaji yao. Aliandika madai kwa Shirika la Taifa la Gesi na Petroli na kuuliza masuala kadhaa wa kadhaa. Siku hiyo hiyo lilipofika dai lake akapigiwa simu na huduma ya upatikanaji wa gesi ya kupikia ikarekebishwa.

Nae Madhu Bhaduri alikuwa na malalamiko ya kuziba kwa karo katika eneo la nyumba anakokaa mama yake na kusababisha uchafu na mbu. Hatua kadhaa zilishindikana mpaka alipopeleka madai kwa kutumia sheria ya kupata taarifa na ndipo hatua ikachukuliwa na karo hiyo ikazibuliwa kwa kuingia mkuu mwenyewe na kusimamia suala hilo.

Kwa kutumia mifano hiyo tunaona jinsi gani uwepo wa haki ya kupata taarifa au haki ya kujua kunakoweza kuwa na fadia kwa jamii, kuhimiza uwazi, kuondosha umangi meza na kukuza demokrasia maana wanyonge nao pia wanaweza kupata haki na huduma zinazowastahikia.

Wakati tunasherehekea leo hii siku ya kupata taarifa The International Day of the Right to Know basi pia tuongeze kasi yetu katika kusimamia kutandikwa sheria ya haki ya kupata taarifa Right to Information Act au Freedom to Information Act. Hapana shaka tutakuwa na Zanzibar na Tanzania njema zaidi

Tuna vitu vingi vya kuuliza serikalini ambavyo kwavyo hivi hivi hatupati taarifa zake hata tukifanya nini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.