Na Mwandishi wetu
BODI ya Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDB), imesema kuku walioingizwa na kuuzwa katika mitaa mbali mbali ya Zanzibar kutoka Dubai kuwa ni salama kiafya.
Akizungumza na gazeti hili, Mrajis wa Bodi hiyo, Dk. Burhan Othman Simai alisema baada ya kuingwa nchini wataalamu wa bodi hiyo wamewachunguza na kutobaini kuwepo kwa shaka juu ya afya za wananchi endapo watawatumia.
Katika mitaa kadhaa hivi sasa kumeibuka gari zinazouza minofu ya kuku, ambapo baadhi ya wananchi walianza kuhoji usalama wao endapo watanunua minofu hiyo.
“Wataalamu wetu wamewachunguza na tunawahakikishia wananchi kuwa kuku hao ni salama kwa afya zao endapo watapenda kuwatumia”,alisema Mrajis huyo.
Alisema Bodi ilichukua sampuli ya kuku hao na kuwachunguza katika maabara na kugundua kuwa hawana matatizo yoyote kwa matumizi ya binaadamu na ndipo waliporuhusu kuingizwa nchini.
Burhan alisema kuku hao wazalishwa nchini Brazil na Argentina ambapo hununuliwa kupitia soko la Dubai na baadae kuingizwa Zanzibar huku kampuni inayoingiza minofu hiyo ikifuata taratibu zote kiafya.
Alisema Zanzibar ni eneo tengefu la kibiashara, hivyo haiwezekani kuzuia biashara gani iletwe na ipi isiletwe, ila jambo la umuhimu ni kufuata masharti yaliowekwa juu ya biashara zenyewe ikiwemo usalama kwa watumizi ya binaadamu.
“Serikali imefungua milango ya uwekezaji kwa lengo la kuwapatia maendeleo wananchi wake na kuwaondoshea tatizo la ajira, hivyo kuwepo wawekezaji si jambo baya isipokua jambo la msingi ni kuwepo kwa vyombo vya kusimamia na ndio maana serikali ikaweka Mamlaka ya Uwekezaji (ZIPA) na kuanzisha vyombo vyengine vya usimamizi”, alisema marajis huyo.
Burhan alisema kwa kuwa biashara za Chakula na dawa zipo chini ya bodi hiyo (ZFDP), hivyo inapotokezea muwekezaji yoyote mamlaka ya uwekezaji vitega uchumi (ZIPA) humuelekeza kufika katika bodi ya chakula na dawa kwa lengo la kupata taratibu na masharti yaliyowekwa.
Alisema hadi sasa kuna kampuni tatu zinazofanya biashara kama hizo ikiwemo hiyo inayouza kuku na nyengine mbili zinazojishughulisha na uuzaji wa nyama ya ng’ombe bila ya kuzitaja majina yake.
Hata hivyo Zanzibar Leo ililipata jina la kampuni hiyo inayoingiza minofu ya kuku ambayo ni Malik Faraj Limited, ambapo imeajiliwa Julai mwaka huu.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa kampuni hiyo ya uuzaji wa kuku, Malik Faraj alisema minofu ya kuku wanayoingiza iko salama kwa afya za wananchi.
“Katika biashara kuna mbinu nyingi za kugombea soko, kuna wafanyabiashara wengine wakiona soko lao limeanguka huanza kutafuta mbinu za kuwachafulia wengine jambo ambalo ni kinyume na taratibu za kibiashara” ,alisema Mkurugenzi huyo.
Aidha Faraj alisema kampuni yake imeamua kuwekeza Zanzibar kwa lengo la kuwasaidia wazanzibari kuondokana na ukandamizaji uliopo kwa baadhi ya wafanyabiashara kwa kuwauzia wananchi bidhaa mbali mbali kwa bei za juu wakati uwezekano wa kuuza kwa bei nafuu upo.
Aidha alisema kampuni yake kwa sasa inatoa mitaji kwa vijana mbali mbali waliokua tayari kuuza bidhaa zinazozalishwa na kampuni yake sambamba na kulenga kuwaajiri vijana wa kizanzibari wapatao 2,000 ifikapo mwaka 2014 ambao watakua wakifanya kazi katika viwanda mbali mbali vinavyotarajiwa kujengwa na kampuni hiyo.
Habari hii imerejewa ili kurekebisha makosa ambayo yalitokea kwenye taarifa hii iliyochapishwa katika gazeti la jana ukurasa wa kwanza, kwenye aya ya kwanza ambapo badala ya kusema 'ni' salama iliandikwa kwa makosa 'si' salama, ila taarifa nyengine zote kwenye habari hiyo zilikuwa sahihi. Mhariri anaomba radhi wananchi, pamoja na taasisi zote ambazo kwa njia moja au nyengine zimepata usumbufu kutokana na makosa hayo.
CHANZO: ZANZIBAR LEO
No comments:
Post a Comment