Habari za Punde

202 MUYUNI WAPATIWA MATIBABU KUPITIA ZOP

Na Madina Issa

SHEHA wa Shehia ya Muyuni "B" Ali Haji ameipongeza Jumuiya Zanzibar Outreach Program (ZOP) inayoisaidia jamii kwa matibabu ya macho,masikio,pua,koo,presha na sukari kwa kuwapelekea huduma hiyo kijijini kwao.

Akizungumza na wananchi wake katika matibabu ya maradhi hayo,alisema hivi sasa kuna matatizo hayo mengi katika shehia yake.


Sheha huyo aliishauri Jumuia hiyo iendeleze kutoa huduma hiyo kwani inawasaidia kuyajua matatizo yao yanayowakabili.

Hata hivyo amewataka wafanye utaratibu wa kuwasaidia na wagonjwa walokuwepo majumbani kwa kuwafuata kwani wapo wasiojiweza kutokana na hali zao.

Nao wananchi walioshiriki katioka matibabu hayo wameishukuru Jumuia hiyo kwa kuwapa matibabu pamoja na dawa kutokana na maradhi ya mtu aliyokutwa nayo.

Mmoja wa wananchi hao Abdala Salehe Makame kutoka kijiji cha Muyuni aliushukuru uongozi mzima wa ZOP kwa kuweza kwenda kijijini kwao kwa lengo la kupatiwa matibabu ya magonjwa mbali mbali walionayo.

Hata hivyo aliwaomba waendeleze utaratibu huo ili wapate kuwatatulia matatizo walionayo.

Nae Katibu wa jumuia hiyo Naufali Kasim Mohammed, alisema wamepokea kwa furaha pongezi hizo na kuahidi kwamba watakuwa nao bega kwa bega kwani hivi sasa wana mpango wa kukutana na serikali ili waweze kuwasaidia zaidi wananchi wa Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.