Habari za Punde

UONGOZI WA ZANTEL/ETISALAT WAKUTANA NA DK SHEIN KATIKA KUOMBOLEZA

Na Rajab Mkasaba

 Dk Shein akisalimiana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Etisalat, Essa Al Haddaad, walipofika Ikulu kumpa pole Rais.


Dk Shein akizungumza na uongozi wa Bodi wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Etisalat walipofika Ikulu kumpa pole.

UONGOZI wa Kampuni ya ZANTEL ukiongozana na uongozi wa juu wa Kampuni mama ya ETISALAT umemueleza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein kuwa wanaungana na ndugu zao wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla kuomboleza msiba mkubwa uliotokea kufuatia kuzama kwa meli ya MV Spice Islander hivi karibuni.


Uongozi huo ulieleza hayo wakati ulipofika Ikulu mjni Zanzibar kwa lengo la kumpa mkono wa pole Rais Dk. Shein kufuatia msiba huo mkubwa ambao haujawahi kutokezea katika visiwa vya Zanzibar.

Makamu wa Rais wa Kampuni ya ETISALAT Bwana Obaid Hassan Bokisha alimueleza Dk. Shein kuwa uongozi wa Kampuni hizo kwa pamoja umesikitishwa na msiba huo mkubwa na kueleza kuwa wako pamoja na ndugu zao wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla katika kuomboleza msiba huo.

Alieleza kuwa Kampuni hizo kwa pamoja zinatoa mkono wa pole kwa Rais Dk Shein pamoja na viongozi wengine wote na wananchi kwa jumla kutokana na msiba huo na kuwaombea kwa MwenyeziMungu maisha mema peponi wale wote waliopoteza roho zao sanjari na kuwaombea kupona kwa haraka wale waliopata majeraha.

Uongozi huo ulieleza kuwa umesikitishwa kwa kiasi kikubwa na msiba huo na kuahidi kuungana na serikali kwa kuwasaidia wananchi waliopata janga hilo na kuwataka viongozi, wananchi wakiwemo waliopatwa na janga hilo kuwa na subira katika kipindi hichi kigumu cha msiba.

Aidha, uongozi huo ulieleza lengo lake la kusaidia uimarishaji wa sekta ya afya kwa kutoa huduma ya mawasiliano kwa urahisi zaidi kufuatia mradi maalumu uitwao
‘M-Health’utakaoanzishwa kwa mashirikiano ya Kampuni ya ZANTEL, Kampuni ya D- TREE pamoja na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambao utakuwa wa kisasa zaidi.

Uongozi huo ulieleza kuwa teknolojia hiyo itakuwa ni ya kwanza hapa nchini na kueleza kuwa mradi huo utaimarisha huduma za afya kwa jamii ikiwa ni pamoja na kutumia simu za mkono kwa kutatua ya afya hasa lishe ambapo pia, mama wajawazito nao watafaidia.

Pamoja na hayo, uongozi huo umeahidi kuendeleza uimarishaji wa Kampuni zake hizo ili ziweze kutoa huduma zaidi kwa wananchi wa Zanzibar na Tanzania nzima kwa ujumla.

Nae Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Shein alitoa pongezi kwa ujio wa uongozi huo na kueleza kuwa hatua hiyo imewapa faraja viongozi pamoja na wananchi wote wa Zanzibar kwa kuona kuwa Kampuni zao hizo za mawasiliano ziko karibu nao katika kipindi hichi cha msiba.

Dk. Shein alisema kuwa tukio hilo ni kubwa na limesababisha majonzi kwa wananchi walio wengi kwani kila mmoja ameguswa na msiba huo.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alitoa shukurani kwa Kampuni ya ZANTEL pamoja na Kampni mama ya ETISALAT kwa kuwa pamoja katika kuomboleza msiba huo.

Aidha, Dk. Shein alisema kuwa mawasiliano ni jambo muhimu sana katika shughuli mbali mbali na kueleza kuimarikwa kwa Kampuni ya ZANTEL kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha sekta za maendeleo nchini.

Katika maelezo yake pia, Dk. Shein aliueleza uongozi huo kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa Kampuni hizo hapa Zanzibar ili ziweze kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.

Alieleza kuwa Kampuni ya ZANTEL imekuwa na mchango mkubwa hapa Zanzibar na imeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kuimarika kwa maendeleo ya mawasiliano nchini.

Akipongeza azma ya Kampuni ya ZANTEL kusaidia sekta ya afya kimawasiliano, Dk. Shein alisema kuwa kutokana na mikakati ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kupambana na vifo vya akina mama wajawazito na watoto, mradi huo utasaidia kwa kiasi kikubwa.

Alieleza kuwa serikali inapongeza hatua ya Kampuni hizo kwa kuunga mkono juhudi za kuimarisha sekta ya afya katika kutoa huduma za kijamii.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.