Habari za Punde

WANANCHI TUSUBIRI RIPOTI YA TUME - BALOZI SEIF


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na wafiwa wa majimbo ya wilaya ya Wete Kisiwani Pemba alipofanya ziara ya kuwapa pole alipokutana nao katika majengo ya skuli ya gando

Jibu la tatizo na sababu iliyopelekea kuzama kwa M.V Spice Islanders wiki mbili zilizopita litapatikana baada ya kukamilika kwa uchunguzi unaofanywa na Tume ya Watu kumi iliyoundwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dr. Ali Mohamed Shein kufanya uchunguzi huo. 

Akizungumza na Familia za wafiwa wa ajali ya Meli ya M.V Spice Islanders katika Majimbo ya Ole, Kojani na Gando Wilaya ya Wete Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema Tume hiyo itaweka wazi Ripoti itakayohusika na tatizo hilo. Balozi Seif amesema ripoti hiyo itatoa muongozo wa namna ya Taifa na Umma wote utakavyoweza kukabiliana na maafa yatakayotokea siku nyengine zijazo. 


Alisisitiza kwamba Serikali itajitahidi kuona vyombo vya usafiri vinakuwa imara na kamwe haitasita kuzuia chombo chochote kibovu kwa lengo la kulinda usalama wa abiria na mali zao. Balozi Seif ametahadharisha kwamba taratibu lazima zifuatwe na hili litafanikiwa iwapo ushirikiano wa pamoja utapatikana kati ya Wananchi,Serikali pamoja na Taasisi zinazosimamia masuala hayo.

 "Tunachotaka sasa ni kuhakikisha kwamba abiria wanasafiri kwa njia ya usalama, hatutaki meli zijiendee bila ya ukaguzi ’’. Alisema Balozi Seif. Amesema ni vyema Wananchi wakaongeza mashirikiano yao na Serikali ili kuona Sekta ya usafiri inaendelea kutoa huduma kwa uhakika na kuaminika.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliendelea kuwaomba wafiwa kuwa na moyo wa subira kwani subira ni nusu ya amani. Balozi Seif Ali Iddi amekamilisha ziara yake ya kuzifariji familia za wananchi waliofariki kwa ajali ya Meli ya M.V Spice katika Majimbo ya Ole, Kojani na Gando yaliyomo ndani ya Wilaya ya Wete Kisiwania Pemba.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.