Habari za Punde

2764 HAWAJULIKANI WALIPO AJALI YA MV SPICE

Na Mwantanga Ame

SERIKALI ya Zanzibar imesema watu 2,764 wameripotiwa kutoonekana wakiwa hai ama maiti baada ya kutokea ajali ya kuzama meli ya Spice Islander 1, iliyotokea mkondo wa bahari ya Nungwi mwezi uliopita.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, aliyasema hayo jana wakati akitoa taarifa ya serikali juu ya tukio hilo kwa wajumbe wa baraza la Wawakilishi kikao ambacho kinaendelea kufanyika Chukwani Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.


Balozi Seif, alisema idadi hiyo ya watu ilikusanywa hadi kufikia Oktoba 9, mwaka huu baada ya kuziagiza Wilaya na Shehia, kuorodhesha majina ya watu ambao hawajaonekana na wanaosadikiwa walikuwa ndani ya meli hiyo.

Kutokana na orodha hiyo hadi tarehe hiyo ya mwisho watu ambao waliorodhesha wakiwa hawajaonekana kuwa hai ama maiti wamefikia kiwango hicho, lakini imebainika wapo walioorodheshwa zaidi ya mara mbili katika maeneo tofauti ya Unguja na Pemba.

Alisema baada ya ajali hiyo kutokea familia ambazo zilifarijiwa na viongozi mbali mbali wa serikali akiwemo yeye binafsi baada ya tukio hilo ni 273 kati ya familia 337 zilizosajiliwa kwa Wilaya za Unguja na Pemba ambapo kila familia ilipatiwa shilingi 100,000.

Alisema familia zilizobaki zinaendelea kupewa ubani kwa utaratibu maalum ulioandaliwa na serikali na hadi kufikia sasa tayari familia 1,299 zimeshafarijiwa.

Alisema mchango ambao serikali imeupokea kutoka kwa watu mbali mbali hadi sasa umefikia shilingi bilioni 1,002, 775,571 ambazo zimeingizwa katika mfuko wa maafa kwa kufunguliwa akauti maalum katika Benki ya watu wa Zanzibar (PBZ) na serikali imekuwa ikizingatia namna ya fedha hizo zitavyotumika ili kufikia malengo yaliokusudiwa.

Alisema tangu kutokea kwa ajali hiyo serikali imelazimika kutoa mchango wake wa shilingi 100,000,000 na hadi kufikia Septemba 30 mwaka huu imeshatumia shilingi 99,984,386 na fedha hizo hazihusiani na michango iliyotolewa na wadau mbali mbali.

Hata hivyo alikishukuru kikosi cha Uokozi cha Afrika Kusini kwa kuja kutoa mchango wao kusaidia kutafuta miili hiyo lakini kilishindwa kuwafikia kutokana na meli hiyo kuzama kina cha mita 270 hadi 300.

Balozi Seif alisema hivi sasa tayari serikali imeunda Kamati ya watu 10 kuchunguza tukio hilo ambapo inatarajiwa kutoa taarifa yake ndani ya kipindi cha mwezi mmoja ujao.

Kutokana na ajali hiyo Balozi Seif alisema serikali inakabiliwa na changamoto mbali mbali baada ya kubaini kuwepo kwa haja ya kuimarisha suala la mawasiliano wakati wa maafa kutokana na mtandao wa Zantel kuonekana kuzidiwa na kusababisha tatizo la mawasiliano.

Eneo jengine ambalo alieleza litahitaji kuangaliwa ni pamoja na chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Mnazimmoja kutokana na kuwa ni kidogo jambo lililosababisha maiti zilizoshindwa kutambuliwa na jamaa zao kuzikwa haraka kwani hazikuwa na eneo la kuhifadhiwa.

Pia Makamu huyo alisema tatizo la uhaba wa vifaa vya uokozi nalo ni jambo linalohitaji kushughulikiwa kutokana na baadhi ya wazamiaji kushindwa kufikia eneo la ajali kutokana na kukosa vifaa.

Alisema eneo jengine ambalo litahitaji kuangaliwa ni lile linalohusu kuwepo kwa mkakati wa elimu ya kujikinga na maafa ya majini, vifaa na wataalamu kunakosababisha kutokea kwa ajali za mara kwa mara.

Kutokana na hali hiyo Balozi Seif alisema mkakati ambao serikali inakusudia kuuchukua ni kuifanyia marekebisho sheria nambari 2 ya mwaka 2003 ya kukabiliana na maafa ili iendane na mahitaji na mazingira ya hivi sasa.

Eneo jengine alisema ni kutekeleza kikamilifu mpango wa taifa wa kukabiliana na maafa pamoja na Mkakati wa Mawasiliano wakati wa Maafa, kujenga uwezo kitaasisi, kutafuta ushauri wa kitaalamu wa kujikinga na majanga na kufikiria kuanzisha vituo vya uokozi katika maneo ya Unguja na Pemba.

Aidha eneo jengine ambalo alilitaja ni la kuendelea kutoa elimu ya kukabiliana na maafa kwa jamii na kuimarisha Kamati za maafa katika shehia, Wilaya na Taifa na kudhibiti vyombo vya usafiri vya abiria na mizigo vya baharini na nchi kavu ili kuepusha ajali na upotevu wa maisha na mali za wananchi.

Makamu huyo aliwashukuru wadau mbali mbali waliojitolea kushiriki uokozi wa watu hao wakiwemo wananchi wa kijiji cha Nungwi.

Jumla ya watu 203 walifariki dunia kwa ajali hiyo ya kuzama kwa meli na watu 619 walinusurika vifo baada ya kuokolewa na wananchi katika kijiji Cha Nungwi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.