Habari za Punde

SAKATA LA MV SPICE LATIKISA BARAZA - KAMATI YAMTAKA WAZIRI AACHIE NGAZI

Wasema ameshindwa kuwajibika
Mwenyewe asema bado ni mapema
Hamza ataka ‘Business as Usual’ iachwe

Na Mwantanga Ame

KAMATI ya Baraza la Wawakilishi ya kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa, imetoa tamko zito la kumtaka waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Hamad Masoud kujiuzulu kutokana na kufariki zaidi ya watu 200 kulikotokana na kuzama na meli ya Mv Spice Islanders I.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Hamza Hassan Juma alilieleza Baraza la Wawakilishi alipokuwa akitoa maoni ya kamati hiyo, baada ya serikali kuwasilisha taarifa ya tukio hilo.


Mwenyekiti huyo alisema haja ya kujiuzulu kwa kiongozi huyo ipo wazi kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu yake pamoja na kutoa kauli barazani akiwa anashindwa kuzifanyia kazi.

Hamza alisema kilichoonekana katika tukio hilo kuwepo kwa uzembe wa wazi uliofanywa na wahusika wanaohudumia na kusimamia idadi na usalama wa abiria.

Alifahamisha kuwa kabla ya kutokea kwa ajali hiyo ndani, wajumbe wa Baraza hilo walishawahi kupiga kelele namna ya udhibiti wa idadi uingiaji wa abiria melini, lakini waziri huyo amekuwa akitoa jawabu za kubahatisha ambazo hana uhakika nazo na kuonesha kutokujali taarifa zinazotolewa na wananchi kupitia vyombo vya habari ikiwemo magazeti.

Akinukuu baadhi ya majibu aliwahi kutoa waziri huyo mbele ya baraza hilo. Hamza alisema ni pale alipolieleza Baraza kuwa wizara yake kupitia Mamlaka ya Usafiri Baharini imekuwa ikipokea taarifa mbalimbali kuhusiana na usafiri na mwenendo mzima wa vyombo vya baharini.

Alisema waziri huyo aliwahi kuliambia Baraza kwamba wizara ya Miundombinu na Mawasiliano kupitia Mamlaka ya Usafiri Baharini wanachukua hatua zote za kiusalama wa vyombo vya usafiri baharini kabla ya vyombo kufanya safari zake.

Aidha kauli nyengine iliyowahi kutolewa na waziri huyo alisema ni pale alipoeleza kuwa wataendelea kuchukua hatua zote za kiusalama kwa vyombo vyote vinavyofanya safari hizo na kufanya huduma hizo za kusafirisha wananchi ikiwemo kuvikagua na kuvithibitisha juu ya safari zake.

Alisema kwa kauli hizo zilizowahi kutolewa na waziri huyo, kama angelizifuata kusingekuwa na sababu ya kutokea kwa ajali hiyo na kupoteza maisha ya watu.

“Ndio maana kamati yangu imebaini kwamba kuna ubabaishaji mkubwa wa kiutendaji katika wizara hii na kukaa ofisini na kutuletea taarifa za kujifurahisha wao tu na sio uhalisia”, alisema Mwenyekiti huyo.

Mwenyekiti huyo alisema kutokana na uzembe huo uliofanywa na wizara hiyo umeonesha wazi kuwa waziri ameshindwa kusimamia ipasavyo majukumu yake aliyopewa na Rais na kwa mujibu wa sheria zinazoongoza mamlaka ya usafiri wa baharini kuna iupengele kinachomtaka waziri kuunda tume linapotokea jambo kama hilo lakini kazi hiyo imefanywa na Mamlaka nyengine.

“Kwa maana hiyo hapa tunamtaka waziri wa Miundombinu na Mawasiliano ajiuzulu kwa hiari yake ili kuonesha uwajibikaji na asisubiri kuwajibishwa na Rais kwa uzembe wa kutokusimamia majukumu aliyopewa na tunaamini akifanya hivyo itakuwa ni kweli Serikali yetu inawajibika kwa wananchi na hata Mwenyezi Mungu amesema kwamba (kila mchunga ataulizwa kwa anachokichunga ), hiyo ndio demokrasia na utawala bora unavyotaka, kwani demokrasia ni gharama”, alisema Mwenyekiti huyo.

“Muheshimiwa Spika, kama kweli tunataka tuendelee lazima tubadilike kama anavyosema Rais wetu, tusifanye kazi kwa mazoea (Business as usual), kuna mifano mingi ya serikali kuwajibika duniani tangu kuchaguliwa Rais mwanamke huko Brazil, Roshelina mwezi Januari mwaka huu hadi sasa mawaziri wamejiuzulu kwa hiari yao, kutokana na makosa mbali mbali ya taasisi zao, Japan kwa miaka mitano ni mawaziri wakuu watano wamejiuzulu”, alisema Mwenyekiti huyo.

Alifahamisha kuwa Tanzania Rais mstaafu wa Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi alijiuzulu kutokana na vifo vya wafungwa gerezani alipokuwa waziri wa Mambo ya Ndani na sio Mkuu wa Magereza aliyewajibika, wakati wa utawala wa Mwalim Nyerere, na ikiwa Zanzibar italifanya haitakuwa ni jambo geni.

Alisema mfano ulio wazi ni pale baada ya kuzama kwa meli ya MV Fatih, waziri aliahidi wasafiri lazima watatumia vitambulisho lakini inaonekana suala hilo halifanyiki na wanachoona ni kuwapo kwa kuondolewa njiani wajumbe wa Baraza hilo.

Eneo jengine ambalo Mwenyekiti huyo alisema kamati yake haikuridhika nalo katika taarifa ya serikali ni kuhusu kushindwa kwa wazamiaji kutoka Afrika Kusini kwa sababu ya kina kirefu cha maji, huku akihoji walipoitwa ilishindikanaje kuwapa taarifa za kina cha maji katika eneo hilo.

Alisema taarifa za kina cha maji katika eneo hilo zilikuwa zinajulikana baada ya wazamiaji Zanzibar walipojaribu kuzamia eneo hilo waligundua kima cha maji sehemu hiyo ni kiasi mita 300 kabla ya kuja wataalamu hao.

“Tunaitaka serikali tujifunze kutokana na makosa yetu wakati na siku yeyote tutakapohitaji msaada kutoka kwa wenzetu basi tuwape taarifa za kutosha kwa kazi watakayokuja kuifanya ili kuweza na wao kujitayarisha na vifaa na zana zinazostahili na kama uwezo wao utakuwa ni mdogo basi kutujuulisha mapema”, alisema Mwenyekiti huyo.

Akizungumza na Zanzibar Leo Waziri wa wizara ya Miundombinu na Mawasiliano, Hamad Masoud, alisema suala la kujiuzulu bado hajaliona kama analazimika kulifanya kwa hivi sasa kwa vile hayo ni maoni yaliotolewa wajumbe hao.

Alisema yeye binafsi hawezi kuyakataa maoni ya wajumbe hao kwa vile ni haki yao ya msingi lakini kiutendaji bado kuna maeneo ambayo kisheria na mamlaka ya nchi inaweza kuyaangalia kama ana lazimika kujiuzulu.

Akifafanua kauli yake hiyo alisema suala hilo hivi sasa limo katika kufanyiwa uchunguzi na kamati za Usalama ambayo ndio itayoweza kuleta taarifa kama itamhusu yeye kutakiwa kujiuzulu kwa vile chombo hicho ni kikubwa na ndio maana amekiachia kifanye kazi yake.

Hivi karibuni Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na waandishi wa habari akitokea ziarani nchini India, alisema waziri huyo aliwasilisha barua ya kujiuzulu katika chama lakini kulitokea mgawanyiko mkubwa.

Alisema wapo viongozi wa CUF waliotaka waziri huyo ajiuzulu huku wengine wakitaka asuburi tume iliyoundwa na ikibainika anakosa ndio aachie ngazi.

1 comment:

  1. Hapa ndipo ulipo mtihani wa wazanzibari! kama kweli tunataka utawala wa sheria,basi tulipe gharama zake lau kama tunapenda vyama vyetu na viongozi wake, basi tuachie kama ilivyo!..tunajua inauma, hasa kwa vile tuna serekali ya umoja wa kitaifa na ina mda mfupi, lkn. tukumbuke huo hautakua mwisho wa mheshimawa huyo kisiasa bali atakua ameweka'precedent' kusudi na wengine waje wafate nyayo zake!lkn. kubwa zaidi ni kwamba hata mridhi wake atakua kutoka C.U.F sasa kuna tatizo gani?..Tunaelewa hata hayo maoni ya kamati yaliyoletwa barazani yana 'elements za ushabiki kidogo kwani Z.N.Z hatuna utamaduni huo ni vile tu ' kamba mbovu' imekatikia upande wa wenzao. Hata hivyo CUF wafanye maamuzi magumu na sisi tuta waelewa.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.