ZANZIBAR imetajwa kuwa ni miongoni mwa nchi zenye mashirikiano mazuri na China kimaendeleo hasa katika nyanja ya sayansi na teknologia na misaada katika vyombo vya habari.
Akifungua warsha ya teknolojia ya utangazaji kwa nchi zinazoendelea, Mkurugenzi mwendeshaji wa China Radio na Televisheni (CRTV) Li Jinrong, alisema Zanzibar imekuwa ni rafiki na mshirika wa siku nyingi ikilinganishwa na nchi nyengine za Afrika katika ukuzaji wa teknolojia ya habari ambayo ni muhimu kwa dunia ya sasa.
Alisema vyombo vya habari vina wajibu mkubwa wa kuhakikisha vinakwenda sambamba na sayansi na teknolojia kwa lengo la kufikisha ujumbe kwa jamii na kuharakisha maendeleo.
Jinrong ambaye ni Mhandisi, alisisitiza kuwa ushirikiano baina ya China na nchi zinazoendelea za Afrika ni njia moja ya kubadilishana uzoefu wa matumizi yateknolojia ili kuleta uwiano wa mfumo wa dunia wa teknolojia hasa katika vyombo vya habari.
Alisema kwa sasa China imeandaa miradi zaidi kadhaa ikilenga kutoa elimu kwa nchi za Afrika kuhusiana na sayansi na teknolojia kwa vyombo vya radio na televisheni.
Aidha China imefanikiwa katika usambazaji wa mitambo ya masafa mafupi (Short Wave) na masafa ya kati (Medium Wave) pamoja na kutoa mafunzo kwa watendaji wa vyombo vya habari.
Mhandisi Jirong, alifahamisha kuwa lengo la miradi hiyo ni kubadilishana uzoefu wa kiutendaji wa kazi za kiteknolojia pamoja na kudumisha mashirikiano kati yao na nchi nyengine katika tasnia ya habari.
Warsha hiyo ya wiki mbili inayowashirikisha wanahabari kutoka vyombo vya habari vya Afrika ikiwemo Tanzania Bara, Zanzibar, Malawi, Botswana, Congo, Ethiopia, Cambodia na China yenyewe inafanyika mjini Beijing nchini China.
No comments:
Post a Comment