Na Hassan Hamad, OMKR
MAKAMU wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad, amevimwagia sifa vikosi cha serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, jinsi vilivyojidhatiti katika kukabiliana na utoroshwaji wa zao la karafuu kwa njia ya magendo.
Alisema vikosi hivyo vinastahiki sifa kutokana na udhibiti za wao hilo, hali iliyoleta matumaini ya kufikiwa kwa malengo ya ununuzi wa zao hiko kufikia tani 2770 kwa msimu huu.
Maalim Seif alieleza hayo huko, Msuka kisiwani Pemba wakati alipotembelea shughuli za udhibiti wa magendo ya karafuu katika eneo hilo.
Alifahamishwa kwa kiasi kikubwa ameridhishwa na kazi inayofanywa na vikosi hivyo, na kuvitaka kufanyakazi kwa uadilifu na kuzidisha ushirikiano ili kuleta mafanikio katika kulinda rasilimali hiyo muhimu kwa uchumi wa taifa.
Aidha alishauri wakulima za karafuu kuhakikisha wanafanya matumizi sahihi ya fedha wanazozipata baada ya kuuza karafuu, kwa kuimarisha mkaazi yao pamoja na kuwasomesha watoto.
“Nakuombeni sana wakulima, fedha zinazoingia kwenye vijiji vyenu ni nyingi, itumieni fursa hiyo kuendeleza makazi, kuwapatia watoto elimu bora, sio kutafuta tasi wanene na kuongeza majiko”, alisisitiza Maalim Seif.
Wakulima hao waliiomba serikali kupitia Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC), kuangalia uwezekano wa kuweka mizani za kisasa ili kuondokana na malalamiko ya kupunjwa katika upimaji.
Walisema hawana imani na mizani zinazotumiwa hivi sasa kwa madai kuwa ni za kizamani na zimepitiwa na wakati, na kudai kuwa kipimo cha nusu kilo hakionekani katika mizani hizo.
Wamesema wataridhika iwapo serikali itaweka mizani za kisasa zinazosoma uzito na thamani ya uzito huo kama ilivyo kwenye vituo vya mafuta, na kwamba itamfanya kila mkulima aridhike na ukweli utaoonekana kwa uwazi.
Akizungumza kwa niaba ya vikosi hivyo, Hussein Mohammed alimepongeza ushirikiano wanaoupata kutoka kwa viongozi mbali mbali wa kitaifa, na kuahidi kuwa wataendeleza juhudi hizo ili kuhakikisha kuwa karafuu hazitoroshwi nchini.
Katika ziara hiyo Maalim Seif alitembelea vituo kadhaa vya ununuzi wa karafuu vikiwemo Finya, Chonga, Wambaa, Mtambile na Bagamoyo.
Akijibu hoja hizo mbele ya Makamu wa kwanza wa Rais, Naibu Meneja wa ZSTC Pemba, Hamad Khamis Hamad, alisema bado ni mapema kwa shirika hilo kuweza kumudu kupeleka mizani hizo kwa kila kituo, na kwamba wakati ukifika watafanya hivyo.
Alifahamisha kuwa mizani za digital na za kielektroniki haziwezi kutumika kwa sasa kwani ni nyepesi na hazihimili vishindo vya kuwekewa magunia ya karafuu, lakini iwapo zitatumika watahitaji kupata mizani kubwa zaidi zitakazokuwa na uwezo wa kuhimili vishindo.
Meneja huyo alisema mizani zinazotumika sasa hazina matatizo na zilikaguliwa kabla ya kazi ya ununuzi wa karafuu kuanza na zimekuwa zikifanyiwa marekebisho kila haja ya kufanya hivyo inapotokea.
Hadi kufikia mwanzoni mwa wiki hii, zaidi ya tani 1,300 zimeshanunuliwa na ZSTC zikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 20, huku wilaya ya Mkoani ikiongoza kwa kuuza karafuu tani 602.6 zenye thamani ya shilingi 8,899,824,750.
No comments:
Post a Comment